Makumi ya wakimbizi wa DRC huko Uganda waaga dunia kwa kuharisha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i40755-makumi_ya_wakimbizi_wa_drc_huko_uganda_waaga_dunia_kwa_kuharisha
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, makumi ya wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamepoteza maisha baada ya mlipuko wa ugonjwa wa kuharisha kuikumba kambi moja ya wakimbizi magharibi mwa Uganda.
(last modified 2025-11-07T02:31:33+00:00 )
Feb 23, 2018 07:41 UTC
  • Makumi ya wakimbizi wa DRC huko Uganda waaga dunia kwa kuharisha

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, makumi ya wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wamepoteza maisha baada ya mlipuko wa ugonjwa wa kuharisha kuikumba kambi moja ya wakimbizi magharibi mwa Uganda.

Duniya Aslam Khan, msemaji wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) nchini Uganda amesema zaidi ya wakimbizi 26 katika kambi ya Kyangwali karibu na Ziwa Albert wameaga dunia kutokana na ugonjwa huo kati ya Februari 15 na 18.

Zaidi ya Wakongomani elfu 27 wamekimbilia Uganda kupitia Ziwa Albert, wakitoroka mapigano na mauaji katika mkoa wa Kivu Kaskazini, ambako maafisa usalama wanakabiliana na magenge ya waasi.

Kwa mujibu wa UNHCR, maelfu ya wakimbizi wa Kongo wamekusanyika katika mkoa wa Ituri katika mpaka wa nchi hiyo na Uganda, wakiwa na nia ya kuingia Uganda kwenda kutafuta hifadhi, kutokana na kushtadi mapigano kati ya jamii hasimu za eneo hilo.

Wakimbizi wa DRC wakikimbilia Uganda kupitia Ziwa Albert

Taasisi za utoaji misaada ya kibinadamu zinasema mapigano na ukosefu wa usalama na amani mashariki mwa Kongo DR ndani ya miezi miwili iliyopita umewafanya zaidi ya watu laki 2 kukimbia makazi yao, baadhi wakikimbilia nchi jirani za Uganda na Rwanda.

Katika hatua nyingine, polisi ya Rwanda kupitia msemaji wake Theos Badege leo Ijumaa imesema idadi ya wakimbizi wa Kongo DR waliouawa katika maandamano nje ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ni 5 na kwamba wengine 20 wamejeruhiwa. Polisi ya Rwanda hapo jana waliwafyatulia risasi karibu wakimbizi elfu 3 waliokuwa wakipinga hatua ya Umoja wa Mataifa ya kukata mgao wao wa misaada.