Zimbabwe yataka kupanua zaidi ushirikiano wake na Iran
Makamu wa Pili wa Rais wa Zimbabwe amesema kuwa, nchi yake inataka kupanua zaidi ushirikiano wake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kembo Mohadi amesema hayo katika mazungumzo yake na Ahmad Erfanian, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Harare na kusisitiza kwamba, nchi yake ina azma ya kuimarisha zaidi ushirikiano na Iran katika nyuga mbalimbali.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zimbabwe ametoa mkono wa pole na salamu zake za rambi rambi kwa taifa la Iran kufuatia ajali ya ndege iliyotokea hivi karibuni hapa nchini na kuuawa watu wote 66 waliokuwamo ndani yake.
Kembo Mohadi aidha ameitaja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa, rafiki mkongwe wa nchi yake na akaeleza kwamba, kuna haja ya kuchukuliwa hatua zaidi za kustawisha uhusiano kati ya Harare na Tehran.
Amesema pia kuwa, nyanja ambazo nchi yake inapenda kustawisha ushirikiano na Iran ni elimu, teknolojia, sekta ya afya, tiba kilimo na madini.
Kwa upande wake Ahmad Erfanian, balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Harare amesema kuwa, Iran na Zimbabwe zinaweza kutumia uhusiano wao mzuri uliopo na kustawisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali kama za kiuchumi na kibiashara.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikitoa kipaumbele maalumu katika siasa zake za kigeni juu ya uhusiano na nchi za Kiafrika.