Bunge la Somalia lapinga makubaliano ya Imarati na Somaliland
(last modified Tue, 13 Mar 2018 07:35:45 GMT )
Mar 13, 2018 07:35 UTC
  • Bunge la Somalia lapinga makubaliano ya Imarati na Somaliland

Bunge la Federali la Somalia limepiga kura kwa kishindo kupinga makubaliano ya pande tatu kati ya eneo la Somaliland, Umoja wa Falme za Kiarabu na Ethiopia kuhusu bandari ya Berbera, iliyoko katika Ghuba ya Aden.

Katika kikao cha jana, Wabunge 168 kati ya 171 wa bunge hilo walipiga kura kutaka kubatilishwa mapatano hayo, na sasa muswada huo utasubiri sahihi ya rais iwapo utapasishwa na Bunge la Seneti la nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Mapema mwezi huu, shirika la Dubai la DP World linalosimamia na kuendesha bandari hiyo ambayo ndio kubwa zaidi eneo la Somaliland, lilitangaza kuwa litachukua asilimia 51 ya hisa za bandari hiyo, mwenyeji Somaliland asilimia 30, huku Ethiopia ikiuziwa asilimia 19.

Machi 2, Waziri wa Bandari na Usafiri wa Baharini wa Somalia alitoa taarifa akiwa mjini Mogadishu na kupinga vikali makubaliano hayo ya Imarati, Somaliland na Ethiopia kuhusu bandari hiyo ya kistratajia.

Ramani ya Somalia

Sio vibaya kukumbusha hapa kuwa, mwaka uliopita, mpango wa Imarati wa kutaka kujenga kambi yake ya kijeshi huko Somaliland ulipingwa vikali na serikali ya Mogadishu na nchi jirani zikiwemo Ethiopia na Djibouti.

Jamhuri ya Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991 na kisha kuitangaza Hargeisa kuwa mji  mkuu wake.