Upinzani Sudan Kusini wataka mazungumzo ya amani yafanyike Ethiopia
(last modified Tue, 20 Mar 2018 15:03:50 GMT )
Mar 20, 2018 15:03 UTC
  • Upinzani Sudan Kusini wataka mazungumzo ya amani yafanyike Ethiopia

Mrengo mkuu wa upinzani nchini Sudan Kusini umepinga mashinikizo ya serikali ya Juba ya kuitaka Jumuiya ya Maendeleo ya Kiserikali ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD ibadilishe sehemu ya kufanyika mazungumzo ya amani kutoka Addis Ababa, Ethiopia.

Peter Oyoyo Kleta, naibu mjumbe wa chama cha upinzani cha SPLM/AIO nchini Tanzania amesema mazungumzo hayo inapasa yafanyike Addis Ababa, na kuyapeleka kwengine ni kuhatarisha maisha ya wakuu wa upinzani wanaoongozwa na Riek Machar.

Amesema serikali ya Juba inakula njama ya kuwaua, kuwakamata au kuwahadaa wakuu wa mrengo huo wa upinzani kwa kisingizio kuwa Ethiopia sio pahala salama kwa sasa pa kufanyika mazungumzo hayo.

Mjumbe huyo wa upinzani amesema serikali ya Juba inataka kuvuruga mchakato wa kupatikana amani ya kudumu kwa kutaka mazungumzo hayo yapelekwe sehemu nyingine badala ya Addis Ababa. Eneo la Oromia na viunga vyake nchini Ethiopia limekuwa katika hali ya taharuki na mchafukoge, tangu Hailemariam Desalegn, ajiuzulu wadhifa wake wa uwaziri mkuu. 

Rais Salva Kiir na Riek Machar

Mapema mwezi huu, IGAD ilisema kuwa inaunga mkono hatua ya kuwekewa vikwazo viongozi na shakhsia wote wanaokwamisha jitihada za kupatiwa ufumbuzi mgogoro nchini Sudan Kusini.

Sudan Kusini ambayo ilijitenga na Sudan mwaka 2011, ilitumbukia katika vita vya ndani mwaka 2013, baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake. Vita hivyo vimesababisha mauaji ya maelfu ya watu na kulazimisha mamilioni ya wengine kuwa wakimbizi.