ANC yamkana Jacob Zuma katika kesi ya ufisadi
Katibu Mkuu wa chama cha ANC, Ace Magashule amesema kuwa, chama hicho tawala cha Afrika Kusini hakihusiki na vitendo vya ufisadi vinavyodaiwa kufanywa na rais wa zamani wa nchi hiyo, Jacob Zuma.
Amesema, chama hicho hakitamuunga mkono Jacob Zuma katika kesi ya ufisadi inayomkabili, lakini wanachama wa chama hicho wako huru kumtetea na kumuunga mkono kwa sharti wasifanye hivyo kwa jina la chama.
Jacob Zuma anatarajiwa kupandishwa kizimbani tarehe 6 mwezi ujao wa Aprili katika mahakama kuu ya Durban kwa tuhuma za ufisadi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jioni, Magashule alithibitisha habari zinazosema kuwa, Zuma amehudhuria kikao cha Kamati Kuu ya ANC (NEC) kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini Cape Town. Alisema, alishiriki kikao hicho kama kiongozi mstaafu kwa mara ya kwanza. Marais wote wa zamani wanachama wa chama hicho, wanashiriki kwenye vikao vya kamati kuu kama viongozi wastaafu.
Hata hivyo Magashule amekuwa akisema mara kwa mara kwamba mtu yeyote hapaswi kuangaliwa kwa jicho la mkosa na mhalifu hadi pale kosa lake litakapothibitika. Amesema, madai yatabakia kuwa madai tu. Hatumuungi mkono wala kumtetea yeyote.
Takriban siku kumi zilizopita, mwendesha mashtaka mkuu wa Afrika Kusini alisema kuwa, Jacob Zuma lazima atapandishwa kizimbani. Alisema, mahakama ndiyo njia bora zaidi ya kutatua suala hilo.
Mwezi uliopita Jacob Zuma (74) alilazimishwa kujiuzulu urais wa Afrika Kusini na chama chake cha ANC na nafasi yake kuchukuliwa na Cyril Ramaphosa.