UNHCR: Waethiopia waliokimbilia hifadhi Kenya wakumbwa na masaibu
(last modified Thu, 29 Mar 2018 06:31:06 GMT )
Mar 29, 2018 06:31 UTC
  • UNHCR: Waethiopia waliokimbilia hifadhi Kenya wakumbwa na masaibu

Maelfu ya wakimbizi wa Ethiopia waliokimbilia hifadhi nchi jirani ya Kenya hivi sasa wanakabiliwa na tatizo kubwa la kukidhi mahitaji yao ya msingi, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR.

UNHCR inasema ingawa inashirikiana na serikali ya Kenya na wadau wengine kutoa msaada wa dharura kwa wakimbizi hao lakini kibarua ni kigumu.

Burton Wagacha mratibu wa dharura wa UNHCR anasema, “changamoto iliyopo sasa ni chakula, wamewasili bila kitu chochote na wanahitaji vitu vya msingi kama vyombo vya kupikia, wanahitaji maji, wanahitaji malazi na wanahitaji huduma za afya”.

Ameongeza kuwa ingawa jamii ya Halakano karibu na kambi hiyo imejitolea kuwasaidia wakimbizi wanaowasili hali bado ni ngumu.

Hivi karibuni Katibu Mkuu wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Kenya alitangaza kuwa, wakimbizi wapatao 10,000 kutoka Ethiopia wameingia nchini humo tangu kuanza mwezi huu wa Machi.

Abbas Gullet amewaambia waandishi wa habari kwamba, raia 9,667 kutoka Ethiopia wameingia nchini Kenya mwezi huu pekee wa Machi wakikimbia ukosefu wa amani unaoshuhudiwa katika nchi yao.

Hayo yanajiri wakati ambao mwezi uliopita, serikali ya Ethiopia ilitangaza hali ya hatari nchini humo siku moja baada ya kujiuzulu Hailemariam Desalegn Waziri Mkuu wa nchi hiyo.

Viongozi wa Ethiopia wamesema kuwa hali ya hatari imetangazwa nchini humo kufuatia pendekezo la serikali kwa lengo la kulinda katiba na kuzuia kuzuka machafuko nchini humo.