Apr 01, 2018 04:12 UTC
  • Zaidi ya watu 1000 watiwa mbaroni nchini Ethiopia

Watu elfu moja na 107 wametiwa mbaroni nchini Ethiopia kwa tuhuma za kuvunja sheria za hali ya hatari nchini humo.

Vyombo vya habari vya serikali ya Ethiopia, jana Jumamosi vilitangaza kuwa, watu 1,107 wameshatiwa mbaroni nchini humo tangu ilipotangazwa hali ya hatari tarehe 16 Februari mwaka huu hadi hivi sasa.

Hailemariam Desalegn, waziri mkuu wa zamani wa Ethiopia ambaye amelazimishwa kujiuzulu na maandamano ya wananchi

 

Vyombo hivyo vya serikali ya Ethiopia vimeongeza kuwa, watu hao wanatuhumiwa kushambulia raia na maafisa wa kulinda usalama pamoja na kuchoma moto nyumba za watu na taasisi za fedha na kuharibu mali za serikali na kufunga barabara.

Hali ya hatari ilitangazwa tarehe 16 Februari 2018 nchini Ethiopia baada ya maandamano makubwa ya wananchi kumlazimisha waziri mkuu wa nchi hiyo Hailemariam Desalegn kujiuzulu.

Siku ya Ijumaa ya tarehe 2 Machi mwaka huu, bunge la Ethiopia lilipasisha rasmi hali ya hatari na amri ya kutotoka nje ili kukabiliana na malalamiko ya wananchi dhidi ya serikali.

Abiy Ahmed, waziri mkuu mpya wa Ethiopia

 

Hailemariam Desalegn amelazimika kujiuzulu baada ya maandamano ya miaka miwili ya wananchi kupinga vitendo vya serikali sambamba na kuongezeka mivutano ndani ya chama tawala cha EPRDF ambacho kimemteua Abiy Ahmed kushika nafasi ya waziri mkuu iliyoachwa wazi na Desalegn.

Abiy Ahmed anatarajiwa kuapishwa mwanzoni mwa mwezi huu wa Aprili kuwa Waziri Mkuu rasmi wa Ethiopia.

Tags