Kesi ya Jacob Zuma yaakhirishwa hadi Juni 8
Kesi inayomkabili Jacob Zuma Rais wa zamani wa Afrika Kusini ya ufisadi wa mali ya umma unaohusiana na kashfa ya silaha jana iliakhirishwa na sasa inatarajiwa kusikilizwa tena Juuni 8 mwaka huu.
Jana Zuma alipandishwa kizimbani katika Mahakama Kuu ya Durban akikabiliwa na tuhuma za ufisadi wa mali ya umma unaohusiana na kashfa ya silaha, hata hivyo baada ya dakika kumi na tano tu tangu kuanza kikao hicho, kesi hiyo iliakhirishwa na sasa itasikilizwa tena Juni nane.
Mawakili wa Jacob Zuma waliomba kuakhirishwa kesi hiyo hadi Juni nane wakisema kuwa, wanahitaji muda zaidi kwa ajili ya kukusanya nyaraka na ushahidi.
Zuma ambaye akipatikana na hatia anaweza kufungwa hadi miaka 15 jela, alisema jana alipowasili mahakamani mjini Durban kwamba, atathibitisha kwamba, hana hatia.
Mwezi uliopita Idara ya Taifa ya Mashtaka nchini Afrika Kusini (NPA) ilitangaza kuwa itamfikisha mahakamani Jacob Zuma kwa tuhuma 16 zikiwemo za udanganyifu, ufisadi na kutakatisha fedha haramu.
Kesi ya Zuma inatambuliwa kuwa ni ya aina yake barani Afrika ambako ni mara chache sana kwa viongozi na wanasiasa wa vyama tawala kupandishwa kizimbani kwa tuhuma kama za ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.
Jacob Zuma ambaye aliiongoza Afrika Kusini kwa miaka 9, alilazimika kujiuzulu mwezi Februari mwaka huu kutokana na mashinikizo makubwa ndani ya chama chake tawala cha ANC.