Apr 07, 2018 07:53 UTC
  • Watu 6 wauawa katika shambulizi la bomu Mogadishu, Somalia

Kwa akali watu sita wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa kufuatia milipuko pacha ya mabomu iliyotokea katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu jana Ijumaa.

Duru za usalama nchini humo zimeripotiwa kuwa, bomu la kwanza lililokuwa limetegwa kwenye gari liliripuka katika makutano ya barabara ya km4 karibu na Uwanja wa Ndege wa Aden Abdulle.

Habari zaidi zinasema kuwa, mlipuko wa pili ulitokea saa moja baadaye karibu na kituo cha upekuzi wa usalama katika eneo la Sei Piano, viungani mwa Mogadishu, katika makutano ya barabara ya Banadir, dakika chache baada ya kumalizika Sala ya Ijumaa.

Askari wawili wa Jeshi la Somalia ni miongoni mwa watu waliouawa kwenye mashambulizi hayo pacha, ambayo genge la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limekiri kutekeleza.

Hujuma ya kigaidi mjini Mogadishu

Mwishoni mwa mwezi uliopita, watu 14 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya mlipuko wa bomu la kutegwa garini kutokea jirani na hoteli moja mjini Mogadishu. 

Harakati za wanamgambo wa al-Shabbab zimeifanya Somalia izidi kukabiliwa na ukosefu wa amani. 

Tags