Apr 10, 2018 07:34 UTC
  • Watu 6 wauawa mbugani Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Askari watano na dereva mmoja wameuawa katika Mbuga ya Wanyamapori ya Virunga huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Serikali ya Kongo DR imethibitisha kutokea mauaji hayo na kuongeza kuwa, askari mwingine wa kulinda mbuga hiyo amejeruhiwa vibaya katika hujuma hiyo iliyotekelezwa na watu wasiojulikana.

Hakuna kundi lolote la waasi lililotangaza kuhusika na shambulizi hilo la jana Jumatatu.

Mbuga hiyo ya kitaifa ambayo ilitajwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kama moja ya turathi muhimu duniani, ina robo ya sokwe wachache wa milimani waliobakia duniani kwa sasa.

Wapiganaji wa mwituni wa DRC

Mwishoni mwa mwezi uliopita, waasi wenye silaha waliwauwa raia wasiopungua 11 katika shambulio jingine kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Watu wasiopungua elfu moja wameshauliwa na magenge ya waasi wanaobeba silaha mashariki mwa Kongo DR tokea mwaka 2014 hadi sasa.

Tags