Mugabe aitwa bungeni ajieleze kuhusu faili la ufisadi wa fedha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43394-mugabe_aitwa_bungeni_ajieleze_kuhusu_faili_la_ufisadi_wa_fedha
Rais wa Zamani wa Zimbabwe, Robert Gabriel Mugabe ametakiwa kufika bungeni kwa ajili ya kutoa ushahidi kuhusiana na madai ya ufisadi wa fedha yaliyofanywa na serikali yake.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 20, 2018 10:00 UTC
  • Mugabe aitwa bungeni ajieleze kuhusu faili la ufisadi wa fedha

Rais wa Zamani wa Zimbabwe, Robert Gabriel Mugabe ametakiwa kufika bungeni kwa ajili ya kutoa ushahidi kuhusiana na madai ya ufisadi wa fedha yaliyofanywa na serikali yake.

Taarifa iliyotolewa na Temba Mliswa, mkuu wa kamati ya nishati na madini katika bunge la Zimbabwe imesema kuwa, tarehe tisa mwezi ujao wa Mei, imeainishwa kuwa siku ya rais huyo wa zamani wa nchi hiyo kufika bungeni na kutoa ushahidi kuhusiana na madai hayo ya ufisadi. Robert Mugabe alikuwa rais wa Zimbabwe tangu mwaka 1980 wakati nchi hiyo ilipojipatia uhuru kutoka kwa mkoloni mkongwe ya Ulaya yaani Uingereza na kubakia madarakani kwa muda wa miaka 37.

Mugabe akiwa na mkewe Grace

Hata hivyo alilazimika kujiuzulu tarehe 21 Novemba mwaka jana baada ya jeshi la nchi hiyo kumlazimisha kujiuzulu. Kuna madai kuwa, mwanasiasa huyo mkongwe alipatwa na hatima hiyo kufuatia azma yake ya kutaka kumuainisha mke wake, Grace Mugabe kuwa mrithi wake wa urais, suala ambalo liliwakera maveterani jeshini. Baada ya Mugabe kujiuzulu, nafasi yake ilichukuliwa na Emmerson Mnangagwa, makamu wake wa rais wa zamani ambaye alimfuta kazi baada ya kuzuka tetesi kwamba alikuwa anafanya kampeni za kuwa rais baada yake.