Machafuko ya Afrika Kusini yamlazimisha Ramaphosa kukatisha ziara yake UK
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i43410-machafuko_ya_afrika_kusini_yamlazimisha_ramaphosa_kukatisha_ziara_yake_uk
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amelazimika kukatisha ziara yake nchini Uingereza na kurejea nyumbani ili kwenda kukabiliana na machafuko.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 20, 2018 23:07 UTC
  • Machafuko ya Afrika Kusini yamlazimisha Ramaphosa kukatisha ziara yake UK

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini amelazimika kukatisha ziara yake nchini Uingereza na kurejea nyumbani ili kwenda kukabiliana na machafuko.

Maandamano ya watu wasio na kazi, wanaotaka makazi mazuri, barabara na huduma nzuri za afya mara nyingi huishia kwenye machafuko na mapigano na polisi katika nchi hiyo ambayo imekumbwa na ukuaji dhaifu wa kiuchumi na idadi kubwa ya ukosefu wa ajira.

Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May

 

Hata hivyo maandamano ya hivi sasa ya Jimbo la Kaskazini Magharibi ni ya kwanza makubwa tangu Ramaphosa alipochukua madaraka ya Afrika Kusini mwezi Februari mwaka huu.

Machafuko hayo yaliyopewa jina la "maandamano ya kulalamikia huduma" yamekuwa yakitokea mara kwa mara na kwa miaka mingi sasa nchini Afrika Kusini.

Maandamano ya hivi sasa yalianza siku ya Jumatano huku wakazi wa jimbo hilo wakishinikiza kujiuzulu mkuu wake, Supra Mahumapelo ambaye ni mwanachama wa chama cha ANC cha Rais Ramaphosa.

Ramaphosa amewataka watu kuwa watulivu kama ambavyo amewahimiza polisi wajitahidi kukwepa kutumia nguvu kadiri wanavyoweza.

Polisi wa Afrika Kusini

 

Rais Ramaphosa alitarajiwa kurudi nchini kwake jana Ijumaa kutoka mjini London ambako alikwenda kushiriki kikao cha Jumuiya ya Madola.

Vyombo vya habari vya Afrika Kusini vimetangaza kuwa basi moja limechomwa moto, magari yamepigwa mawe na barabara zimefungwa na waandamanaji wanaoshinikiza mkuu wa jimbo hilo Mahumapelo kujiuzulu kutokana na kushindwa kutoa huduma zinazotakiwa na wakazi wa jimbo hilo.