Apr 22, 2018 14:01 UTC
  • Mashambulizi pacha ya mabomu yaua kadhaa msikitini Nigeria

Mashambulizi pacha ya mabomu yameua waumini watatu wa Kiislamu msikitini katika mji wa Bama jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Baba Shehu Gulumba, Mwenyekiti wa Serikali ya Mitaa ya Bama amenukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa, mashambuizi hayo yanayoaminika kuwa ya kigaidi yamefanyika wakati waumini wa Kiislamu walipokuwa wamekusanyika kwa ajili ya Sala ya alfajiri.

Habari zinasema kuwa, mwanaume na mwanamke waliokuwa wamejifunga mabomu waliingia msikitini hapo wakati wa Sala ya alfajiri na kujilipua na kusababisha taharuki na mkanyagano.

Duru za kijeshi katika eneo hilo zimethibitisha kutokea hujuma hiyo na kuongeza kuwa, watu wengine tisa wamejeruhiwa, na kwamba baadhi yao wamepelekwa katika eneo la Maiduguri, kwa ajili ya matibabu zaidi.

Majeruhi wakikimbizwa hospitalini kwa ambulensi

Japokuwa genge la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram halijatoa tamko lolote hadi sasa la kutangaza kuhusika na jinai hiyo au la, lakini kundi hilo lililoanzisha uasi mwaka 2009 kwa madai ya kupinga elimu zinazotoka Magharibi huwa kwa kawaida linawatumia watu wanaojiripua wakiwemo wanawake na wasichana kufanya mashambulio ya aina hiyo, katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu kama misikitini na masokoni.

Mapema mwaka huu, gaidi wa kundi la kitakfiri la Boko Haram aliyejifunga bomu mwilini alijiripua na kuua watu wasiopungua 14 ndani ya msikiti mmoja katika mji wa Gamboru ulioko kwenye jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Tags