Wanane wauawa na kujeruhiwa katika mripuko wa bomu mjini Derna, Libya
Watu wanane wameuawa na kujeruhiwa kwenye mripuko wa bomu uliotokea katika mji wa Derna wa mashariki mwa Libya.
Khalid Muhammad, afisa wa kikosi cha operesheni cha Jeshi la Taifa la Libya amesema kuwa, wanajeshi wanne wameuawa baada ya kuripukiwa na bomu la pembeni mwa barabara katika aneo la al-Zohr al-Homr, kusini mwa mji wa Derna na wengine wanne wamejeruhiwa.
Amesisitiza kuwa, hatari kubwa iliyoko mjini humo ni mabomu ya kutegwa ardhini hasa kwa kuzingatia kuwa, magenge ya kigaidi yana maficho yao katika maeneo mengi ya Derna.

Wakati huo huo Jeshi la Taifa la Libya limetangaza kuteka kambi ya kundi la kigaidi la Ansar al Sharia lenye uhusiano wa karibu na genge la kigaidi la Daesh ISIS, kusini magharibi mwa mji wa Derna.
Operesheni za Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali Khalifa Haftar zilianza Jumatatu ya tarehe 7 mwezi huu wa Mei 2018 kwa ajili ya kuukomboa mji wa Derna wa mashariki mwa Libya.
Tangu mwezi Februari 2011 hadi hivi sasa mji wa Derna uko mikononi mwa kundi la Baraza la Mujahid wa Derna lenye uhusiano na mtandao wa al Qaida.