Tanzania kuwachunguza askari wake waliobaka DRC
Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema Tanzania imeshaandaa timu ya uchunguzi ambayo itasafiri kwenda nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kuchunguza madai kuwa askari wake walio katika kikosi cha Umoja wa Mataifa walihusika na unyanyasaji wa kingono.
Farhan Haq amesema Ujumbe wa Kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York umetangaza uamuzi huo baada ya kikao na Idara ya Usaidizi kwa ajili ya vitengo vya Umoja wa Mataifa katika nchi mbalimbali. Haq amesema Umoja wa Mataifa unaishauri Tanzania kuendesha uchunguzi huo kwa ushirikiano na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Usimamizi wa masuala ya ndani (OIOS).
Haq ameongeza kwamba miongoni mwa wanawake 11 wanaodaiwa kuwa wahanga wa ukatili huo wa askari Watanzania, sita walikuwa wenye umri wa chini ya miaka 18.
Aidha, ameeleza zaidi kwamba saba wameshajifungua na wengine wanne bado wako na ujauzito, na kwamba wote sasa hivi wanasaidiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF ambalo limetuma timu maalum kwa ajili yao.
Tuhuma hizo zilitangazwa Jumatatu hii na msemaji wa Umoja wa Mataifa. Askari wote wa kikosi cha Tanzania nchini DRC wamezuiliwa kambini uchunguzi ukiendelea. Vitendo hivyo vyote vimeripotiwa katika kijiji cha Mavivi mashariki mwa DRC karibu na Beni. Umoja wa Mataifa una askari elfu 18 katika kikosi chake cha kulinda amani DRC
Askari wa Umoja wa Mataifa kote duniani wamekumbwa na kashfa za ubakaji na ngono, na mwaka 2015 kulikuwa na kesi 69 zilizoripotiwa.