Jeshi la Madagascar latishia 'kuzima mgogoro wa kisiasa'
Waziri wa Ulinzi wa Madagascar ametishia kuwa, ikilazimu, jeshi la nchi hiyo litaingilia kati iwapo serikali na upinzani zitashindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaoshuhudiwa nchini humo kwa muda sasa.
Beni Xavier Rasolofonirina amezitaka pande hasimu za kisiasa nchini humo ziupatie ufumbuzi mgogoro huo haraka iwezekanavyo, ingawaje hajatoa muhula wa kufanyika jambo hilo, au kufafanua ni jinsi gani jeshi la nchi hiyo litaingilia kati katika mzozo huo.
Ijumaa iliyopita, Mahakama ya Katiba nchini Madagascar ilimuagiza Rais Hery Rajaonarimampianina wa nchi hiyo kuvunja serikali ya sasa na kuunda serikali ya muungano wa kitaifa itakayojumuisha Waziri Mkuu anayekubaliwa na pande zote hasimu za kisiasa ndani ya siku saba, kwa lengo la kutamatisha mgogoro wa kisiasa unaoshuhudiwa katika kisiwa hicho tangu mwezi Aprili mwaka huu.
Hata hivyo Rais Hery Rajaonarimampianina ameonekana kutoridhia uamuzi huo wa mahakama, na hivyo kuufanya mgogoro wa kisiasa katika kisiwa hicho cha kusini mashariki mwa bara Afrika uzidi kutokota.

Mahakama ya Katiba ya Madagascar inataka uundwaji wa serikali hiyo uendane na matokeo ya uchaguzi wa mwisho wa Bunge, na kwamba serikali hiyo ya muungano itatwikwa jukumu la kuandaa uchaguzi wa mapema ambao unapaswa kufanyika kati ya sasa na mwezi Septemba mwaka huu.
Tangu tarehe 21 Aprili, wapinzani wa Rais Rajaonarimampianina wamekuwa wakifanya maandamano wakitaka kubatilishwa sheria za uchaguzi zilizopasishwa hivi karibuni ambazo walizitaja kuwa na upendeleo, sanjari na kumtaka rais huyo ajiuzulu.