Waziri Mkuu wa Madagascar atangaza kujiuzulu
Waziri Mkuu wa Madagascar, Olivier Mahafaly Solonandrasana ametangaza kujiuzulu wadhifa wake leo Jumatatu, ikiwa ni katika kufuata agizo la mahakama la kutaka kuundwa serikali mpya ya muungano wa kitaifa kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaoendelea kutokota katika kisiwa hicho.
Mahafaly amewaambia waandishi wa habari katika ofisi yake kuwa, "Nimekubali agizo hilo pasina masharti yoyote kwa kuwa sitaki kuwa kizingiti katika upatikanaji wa suluhisho. Nimekabidhi barua yangu ya kujiuzulu bila kushurutishwa au majuto yoyote."
Waziri Mkuu wa Madagascar ametangaza kujiuzulu siku chache baada ya Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo kutishia kuwa, ikilazimu, jeshi la nchi hiyo litaingilia kati iwapo pande mbili yaani serikali na mrengo wa upinzani zitashindwa kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa unaoshuhudiwa nchini humo kwa muda sasa.

Wakati huo huo, Mahakama ya Katiba nchini Madagascar imeagiza kuwa, Waziri Mkuu mpya anayekubaliwa na pande zote hasimu za kisiasa ateuliwe kufikia Juni 12, ingawaje awali ilikuwa imeagiza kufikia Juni 5 sambamba na kuunda serikali mpya ya muungano.
Hata hivyo Rais Hery Rajaonarimampianina ameonekana kutoridhia uamuzi huo wa mahakama, na hivyo kuufanya mgogoro wa kisiasa katika kisiwa hicho cha kusini mashariki mwa bara Afrika uzidi kutokota.
Tangu tarehe 21 Aprili, wapinzani wa Rais Rajaonarimampianina wamekuwa wakifanya maandamano wakitaka kubatilishwa sheria za uchaguzi zilizopasishwa hivi karibuni ambazo walizitaja kuwa na upendeleo, sanjari na kumtaka rais huyo ajiuzulu.