Upinzani Ivory Coast: Hatutaruhusu Ouattara agombee muhula wa tatu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i45426-upinzani_ivory_coast_hatutaruhusu_ouattara_agombee_muhula_wa_tatu
Muungano wa upinzani nchini Ivory Coast umesema hautaruhusu mpango wowote wa kumruhusu Rais Alassane Ouattara wa nchi hiyo kugombea muhula wa tatu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Jun 05, 2018 03:07 UTC
  • Upinzani Ivory Coast: Hatutaruhusu Ouattara agombee muhula wa tatu

Muungano wa upinzani nchini Ivory Coast umesema hautaruhusu mpango wowote wa kumruhusu Rais Alassane Ouattara wa nchi hiyo kugombea muhula wa tatu.

Mwenyekiti wa muungano huo unaofahamika kama Together for Democracy and Sovereignty (EDS), Georges Armand Ouegnin ametaja matamshi ya hivi karibuni ya Rais Ouattara kwamba anaweza kugombea muhula wa tatu kama uchokozi wa wazi dhidi ya wananchi wa Kodivaa. 

Amesisitiza kuwa, njama yoyote ya Ouattara ya kugombea muhula wa tatu wa kiti cha rais ni kinyume cha katiba, na ni jambo lisilokubalika na lisiloweza kufikiwa.

Rais wa Ivory Coast akinyayua katiba mpya ya nchi, mwaka 2016

Ouattara ambaye aliingia madarakani baada ya mgogoro wa umwagikaji wa damu wa miezi mitano kati ya mwaka 2010 na 2011, na kwa sasa anahudumu muhula wa pili unaotazamiwa kufikia tamati mwaka 2020.

Katika mahojiano na jarida la Jeune Afrique wiki iliyopita, Rais wa Kodivaa alisema, "Katiba mpya inaniruhusu kugombea mihula miwili kuanzia mwaka 2020, lakini nitatangaza uamuzi wangu wa mwisho wakati huo ukifika, na kwa kutegemea mazingira yatakayokuwepo hapa nchini."