Watu 7 wafa maji katika ajali ya boti kusini mwa Somalia
Watu saba wamethibitishwa kupoteza maisha baada ya boti yao kuzama katika Mto Shabelle, kusini mwa Somalia.
Mashuhuda wa ajali hiyo wameiambia Idhaa ya Risaala kwamba ajali hiyo imetokea katika eneo la Lower Shabelle, kusini mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.
Boti hiyo iliyozama ilikuwa imebeba mizigo na abiria, na ilikuwa ikitoka mji wa Afgoye, yapata kilomita 30 kusini magharibi mwa Mogadishu ikielekea mji wa Qoyoley, umbali wa kilomita 120 kusini mwa mji mkuu huo wa Somalia.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, miongoni mwa walioaga dunia katika ajali hiyo ni mama na watoto wake wanne.

Habari zaidi zinasema kuwa, watu wengine 13 wamejeruhiwa katika ajali hiyo ya kuzama boti mtoni.
Kutokana na hali mbaya ya miundombinu nchini Somalia, haswa barabara hatarishi zenye mashimo, aghalabu ya wananchi wa Somalia hulazimika kutumia usafiri wa majini.