Waziri Mkuu wa Ethiopia anusurika kifo katika hujuma ya mlipuko wa bomu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i46228-waziri_mkuu_wa_ethiopia_anusurika_kifo_katika_hujuma_ya_mlipuko_wa_bomu
Mripuko wa bomu umetokea katikati ya wafuasi wa Waziri Mkuu wa Ethiopia mjini Addis Ababa na ambao ulikuwa umemkusudia kiongozi huyo na kusababisha watu kadhaa kuuawa na wengine kujeruhiwa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2018 09:32 UTC
  • Waziri Mkuu wa Ethiopia anusurika kifo katika hujuma ya mlipuko wa bomu

Mripuko wa bomu umetokea katikati ya wafuasi wa Waziri Mkuu wa Ethiopia mjini Addis Ababa na ambao ulikuwa umemkusudia kiongozi huyo na kusababisha watu kadhaa kuuawa na wengine kujeruhiwa.

Vyombo vya habari vya serikali ya Ethiopia vimetangaza kwamba mripuko huo umetokea leo muda mfupi baada ya kumalizika hotuba ya Abiy Ahmed Ali, Waziri Mkuu wa nchi hiyo mbele ya wafuasi wake. Baada ya tukio hilo, Abiy Ahmed Ali alitangaza kwamba watu kadhaa wameuawa na wengine kujeruhiwa. Aidha Waziri Mkuu wa Ethiopia amesisitiza kwamba, mripuko huo ni njama zilizoshindwa za watu ambao hawataki kuona umoja na mshikamano nchini Ethiopia. Baada ya hujuma hiyo kiongozi huyo aliondolewa katika eneo la tukio kwa ajili ya usalama wake. Baadhi ya duru za habari zinasema kuwa karibu watu 100 wamejeruhiwa, baadhi wakiwa mahututi.

Baada ya kujiri mlipuko huo

Hadi sasa wahusika wa shambulizi hilo bado hawajafahamika kama ambavyo pia idadi kamili ya wahanga bado haijatangazwa. Abiy Ahmed Ali aliteuliwa mwezi Aprili mwaka huu kuwa Waziri Mkuu wa Ethiopia, baada ya mtangulizi wake Hailemariam Desalegn, kujiuzulu nafasi hiyo. Hayo yanajiri katika  hali ambayo kundi la waasi la Patriotic Ginbot7 (PG7) la Ethiopia limetangaza uamuzi wa upande mmoja wa kusimamisha kwa muda usiojulikana operesheni zake zote za utumiaji silaha katika maeneo yote ya nchi.