Jul 06, 2018 13:23 UTC
  • 7 wauawa katika makabiliano kati ya jeshi la Uganda na Kongo DR

Askari wanne na raia watatu wa Uganda wameripotiwa kuuawa katika mapigano makali baina ya vikosi vya majini vya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika maji ya Ziwa Albert.

Donat Kibwana, afisa mkuu wa eneo la Beni, mashariki mwa mkoa wa Kivu Kaskazini nchini Kongo amedai kwamba kikosi cha majini cha DRC kilishambuliwa mapema jana Alkhamisi katika maji ya nchi hiyo na wanajeshi wa majini wa Uganda.

Ameongeza kuwa, boti ya kulinda doria ya Uganda ilizama katika tukio hilo na kusababisha vifo vya wanajeshi wanne wa Uganda na raia watatu.

Afisa huyo wa Kongo DR amebanisha kuwa, askari mmoja wa DRC na raia mmoja wamejeruhiwa katika makabiliano hayo yaliyotokea karibu na kijiji cha Kyavinyonge cha nchi hiyo jirani ya Uganda.

Wavuvi katika Ziwa Albert

Hata hivyo Richard Karemire, msemaji wa jeshi la Uganda ametoa taarifa kinzani, akisisitiza kuwa wanajeshi wa majini wa Uganda ndio walioshambuliwa na watu wasiojulikana ambao walikuwa wamejizatiti kwa silaha karibu na kijiji cha Rwensha katika  pwani ya Uganda.

Amesema katika makabiliano hayo ya jana, askari mmoja wa Uganda ameuawa na mwingine kujeruhiwa.

Jumatano iliyopita, kikosi cha majini cha Uganda kiliwatia mbaroni wavuvi 18 raia wa Kongo kikidai kuwa walikuwa wameingia katika maji ya nchi hiyo ndani ya Ziwa Albert.

Tags