Djibouti yaitaka UN itatue mgogoro wa mpaka wake na Eritrea
Serikali ya Djibouti imeutaka Umoja wa Mataifa uingilie kati na kusuluhisha mgogoro wa mpaka wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika na jirani yake Eritrea.
Mohamed Siad Doualeh, Balozi wa Djibouti katika Umoja wa Mataifa ameliandikia barua Baraza la Usalama la umoja huo akilitaka liongoze jitihada za kimataifa za kuupatia ufumbuzi mgogoro huo kwa njia za amani na kwa kufikiwa muafaka utaokubalika na pande zote mbili.
Mwaka jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilizitaka Eritrea na Djibouti kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa mpaka kati ya nchi mbili hizo kwa njia za amani, na kwa kuheshimu sheria za kimataifa.
Mgogoro huo ulichukua mkondo mpya baada ya Djibouti kuituhumu Eritrea kwamba imezikalia kwa mabavu ardhi na maeneo yanayogombaniwa na nchi mbili hizo, hususan kisiwa na milima ya Dumeira.
Kadhalika Kamisheni ya Umoja wa Afrika AU mwaka jana ilielezea wasiwasi mkubwa ilionao kutokana na kushadidi mvutano kati ya nchi jirani za Eritrea na Djibouti baada ya Qatar kuondoa askari wake waliokuwa wakisimamia amani katika maeneo ya mpakani yanayogombaniwa baina ya nchi mbili hizo za Kiafrika.
Haya yanajiri siku chache baada ya Eritrea na jirani yake mwingine Ethiopia kusaini makubaliano ya amani na kukubaliana kuhitimisha mgogoro wa kidiplomasia na mpaka baina yao uliodumu kwa zaidi ya miongo miwili.