Watu 19 wauawa katika shambulio la wanamgambo kaskazini mashariki mwa Nigeria
(last modified Mon, 20 Aug 2018 07:49:09 GMT )
Aug 20, 2018 07:49 UTC
  • Watu 19 wauawa katika shambulio la wanamgambo kaskazini mashariki mwa Nigeria

Duru za habari zimeripoti kuwa watu 19 wameuliwa katika shambulio lililofanywa na wanamgambo katika kijiji kimoja kilichoko kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Kwa mujibu wa duru za habari katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa Nigeria kijiji cha Mailari kilichoko eneo la Guzamala jimboni humo usiku wa kuamkia jana kilishambuliwa na kundi la wanamgambo waliobeba silaha.

Kwa mujibu wa duru hizo hadi sasa haijajulikana ni kundi gani hasa lililohusika na shambulio hilo lililosababisha vifo vya watu 19.

Magaidi wa kundi la ukufurishaji la Boko Haram

Jimbo la Borno ni kitovu cha mashambulio ya kundi la kigaidi la Boko Haram. Mashambulio ya kundi hilo nchini Nigeria na katika baadhi ya nchi jirani yaliyoanza mwaka 2009, hadi sasa yamesha sababisha watu zaidi elfu 20 kuuawa na wengine zaidi ya milioni mbili na laki sita kupoteza makazi na kulazimika kuwa wakimbizi wa ndani na nje ya nchi.

Juhudi za serikali ya Nigeria za kuliangamiza kundi hilo la kigaidi hadi sasa hazijapata mafanikio kamili.../