Aug 31, 2018 13:56 UTC
  • Pande hasimu CAR zatia saini makubaliano ya amani Khartoum, Sudan

Makundi ya kisiasa na wanamgambo katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wamesaini makubaliano ya amani katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum.

Kanali ya Televisheni ya Russia al-Yaum imetangaza kuwa, pande husika zilizotia saini makubaliano hayo yaliyosimamiwa na Russia na Sudan zimeahidi kufungamana na misingi ya kisiasa ambayo inadhamini usalama na amani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, kutiwa saini hati ya makubaliano ya amani na kuanza mwenendo wa mazungumzo ni jambo la dharura kwa ajili ya kufikiwa amani na uthabiti wa kudumu katika nchi hiyo.

Ukosefu wa amani na usalama katika Jamhuri ya Afrika ya Kati umekwamisha juhudi za serikali ya Rais Faustin-Archange Touadera za kutekeleza mikakati ya ustawi na maendeleo.

Wanamgambo wa Kikristo wa Anti-Balaka wa Jamhuri ya Afrika ya Kati

Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo ni moja ya nchi masikini zaidi duniani, ilitumbukia katika mgogoro wa kisiasa mwaka 2013 baada ya kuondolewa madarakani Rais wa zamani wa nchi hiyo François Bozizé kufuatia hujuma ya waasi wa Seleka nchini humo.

Tangu wakati huo hadi sasa nchi hiyo imekuwa uwanja wa mapigano ya kila uchao kati ya makundi hasimu, hususan lile la Kikristo la Anti-Balaka na kundi la Seleka.

Hali hiyo imezidi kuisababishia matatizo mengi nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati na kuongezeka kila siku idadi ya raia wanaoyakimbia makazi yao wakihofia usalama wa maisha yao.

Tags