Wanachama 10 wa al-Shabaab wauawa na jeshi la Kenya, Lamu
(last modified Mon, 24 Sep 2018 13:57:25 GMT )
Sep 24, 2018 13:57 UTC
  • Wanachama 10 wa al-Shabaab wauawa na jeshi la Kenya, Lamu

Askari wa Kenya wamewaangamiza wanamgambo 10 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika kaunti ya Lamu.

Taarifa iliyosainiwa na Kanali Paul Njuguna, Mkuu wa Kitengo cha Masuala ya Umma cha jeshi hilo amesema askari wa Kenya wamefanikiwa kuwaangamiza wanachama hao wa al-Shabaab katika operesheni iliyofanyika leo asubuhi, ambapo pia wamenasa silaha zao zikiwemo bunduki aina ya AK47.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wanachama wengine kadhaa wa kundi hilo la ukufurishaji wamefanikiwa kutoroka wakiwa na majera na kukimbilia eneo la Taksile, kaskazini mwa Pandanguo.

Kadhalika askari watatu wa Kenya wamejeruhiwa katika operesheni hiyo.

Wanachama wa al-Shabaab, Lamu Kenya

Genge hilo la Kiwahabi limekuwa likifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika kaunti ya Lamu na kutorokea katika msitu wa Boni ulioko katika kaunti hiyo ya pwani ya Kenya.

Jeshi la Ulinzi la Kenya lilianzisha operesheni ya kuusafisha msitu huo iliyopewa jina la 'Operation Linda Boni' baada ya kundi la al-Shabaab kudaiwa kuua askari wapatao 200 wa KDF mwaka 2016.