Sudan Kusini yaiambia UN kuwa makubaliano ya amani hayatakiukwa
Makamu wa Rais wa Sudan Kusini ameuambia mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba makubaliano ya amani ya mara hii yaliyofikiwa hivi karibuni na mahasimu wa kisiasa wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika yatadumu na wana wingi wa matumaini kwamba hayatakiukwa.
Taban Deng Gai aliyasema hayo jana Ijumaa akihutubia mkutano wa UN mjini New York na kubainisha kwamba, serikali ya Juba ipo tayari kuvipokea vikosi vya kieneo ambavyo vitafuatilia na kuhakikisha kuwa makubaliano hayo ya amani yaliyosainiwa kati ya timu ya Rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi, Riek Macha mnamo Septemba 12 yanatekelezwa kikamilifu.
Ameutaka Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kwa ujumla kuwa na imani na matumaini kwamba mapatano hayo hayatakiukwa, akisitiza kuwa serikali ya Juba daima imekuwa ikikaribisha jitihada za kidiplomasia hususan kutoka jumuiya ya kikanda ya IGAD.
Hii ni katika hali ambayo, mapigano kati ya vikosi vya jeshi la serikali ya Sudan Kusini na vya kundi kubwa zaidi la waasi yaliripotiwa kuanza tena kaskazini mwa nchi hiyo, wiki mbili baada ya kusainiwa mkataba wa amani kati ya serikali na upinzani kwa madhumuni ya kuhitimisha vita vya ndani nchini humo.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Riek Machar atateuliwa tena kuwa makamu wa rais wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.
Ripoti iliyotolewa Jumatano iliyopita na taasisi ya London School of Hygiene & Tropical Medicine inasema kwamba, watu karibu laki nne wameuawa katika mapigano ya kikabila nchini Sudan Kusini, tokeo vita hivyo viripuke mwishoni mwa mwaka 2013 hadi sasa.