EU: Uchaguzi wa rais Madagascar ni wenye itibari
(last modified Sat, 10 Nov 2018 08:13:31 GMT )
Nov 10, 2018 08:13 UTC
  • EU: Uchaguzi wa rais Madagascar ni wenye itibari

Waangalizi wa Umoja wa Ulaya katika uchaguzi wa rais uliomalizikka nchini Madagascar wamesema kuwa ukiukaji ulioshuhudiwa katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo ulikuwa mdogo sana.

Cristian Preda, mkuu wa timu ya uangalizi ya EU katika zoezi hilo amesema kuwa, kuhusiana na kile kilichotokea na kushuhudiwa miongoni mwa dosari katika mwenendo wa upigaji kura, kinaweza kuhusishwa na mfumo wa maandalizi pekee na ambacho hakiwezi kuathiri itibari ya uchaguzi wenyewe. Hii ni katika hali ambayo Rais Hery Rajaonarimampianina wa Madagascar na ambaye ameshindwa na mpinzani wake ameelezea kuwepo ukiukaji mkubwa katika uchaguzi huo. 

Vigogo watatu wanaowania kiti cha urais nchini Madagascar 

Madagascar ambayo ilikuwa koloni la zamani la Ufaransa baada ya uchaguzi wa mwaka 2001 ilikumbwa na mgogoro wa kisiasa, uliozua machafuko na mapinduzi ya kijeshi hapo mwaka 2009. Katika tukio hilo rais wa wakati huo, Marc Ravalomanana aliondolewa madarakani na mahala pake kuchukuliwa na Andry Rajoelina. Kiti cha urais wa nchi hiyo ya kisiwa kinagombaniwa na Hery Rajaonarimampianina, Marc Ravalomanana na Andry Rajoelina ambapo duru ya pili ya uchaguzi huo imepangwa kufanyika tarehe 19 Disemba mwaka huu.