Nov 23, 2018 07:56 UTC
  • Boko Haram yawateka nyara watema kuni 50 Nigeria

Kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram limeripotiwa kuwateka nyara makumi ya watu waliokuwa wanatema kuni kaskazini mashariki mwa Nigeria, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Cameroon.

Umar Kachalla, mkuu wa kundi moja la wanamgambo jana Alkhamisi aliliambia shirika la habari la AFP kuwa, wanachama wa Boko Haram waliwateka watu 50 wakikata kuni katika kijiji cha Bulakesa, yapata kilomita 25 kutoka mji wa Gamboru jimboni Borno, Jumamosi iliyopita.

Mashuhuda wanasema mateka wawili walifanikiwa kutoroka, na ndio waliofichua habari za kutekwa wenzao, ambao aghalabu yao ni wakimbizi wa ndani waliokuwa wakiishi kambini, na waliolazimika kuyahama makazi yao kutokana na mashambulizi ya Boko Haram.

Genge hilo la ukufurishaji limeonekana kushadidisha utekaji na mashambulizi yake ya kikatili katika wiki za hivi karibuni. Chini ya wiki mbili zilizopita, genge hilo lilishambulia vijiji kadhaa katika jimbo la Borno, kaskazini mashariki mwa Nigeria na kuua wakulima wasiopungua 16 na kuteka wengine 35.

Mwaka 2014, Boko Haram iliwateka nyara wasichana 276 wa Chibok

Aidha mapema mwezi huu, wapiganaji wa Boko Haram waliuwa watu wasiopungua 15 katika shambulio dhidi ya vijiji vya Kofa na Dalori vilivyoko kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. 

Licha ya serikali ya Nigeria kutangaza mwishoni mwa mwaka 2015 kuwa Boko Haram limesambaratishwa kwa kiasi kikubwa, lakini kundi hilo lingali lina uwezo wa kufanya mashambulizi katika mji wa Maiduguri, maeneo ya karibu yake na katika maeneo mengi ya kaskazini mashariki mwa Nigeria.  

Tags