Bunge la Somalia labatilisha hoja ya kutokuwa na imani na Rais
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50118-bunge_la_somalia_labatilisha_hoja_ya_kutokuwa_na_imani_na_rais
Bunge la Somalia limebatilisha hoja iliyowasilishwa na baadhi ya wabunge waliotaka kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na Rais wa nchi hiyo, Mohammed Abdullahi Farmajo.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 12, 2018 07:41 UTC
  • Bunge la Somalia labatilisha hoja ya kutokuwa na imani na Rais

Bunge la Somalia limebatilisha hoja iliyowasilishwa na baadhi ya wabunge waliotaka kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na Rais wa nchi hiyo, Mohammed Abdullahi Farmajo.

Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, Abdikarim Haji Abdi Buuh amemuandikia barua Spika wa Bunge, Mohamed Mursal, akimtaarifu kuwa hoja hiyo haijakidhi vigezo vya kisheria, kwa kuwa wabunge 14 kati ya 93 waliokuwa wameripotiwa kuwa wameunga mkono hoja hiyo, wamekanusha madai hayo.

Wabunge wapatao 93 walioripotiwa kutaka kuvuliwa madaraka Rais Farmajo, siku ya Jumapili walimkabidhi Mohamed Mursal, Spika wa Bunge la nchi hiyo hoja hiyo, wakimtuhumu rais huyo kwa uhaini baada ya kusaini 'kisiri' makubaliano ya kisiasa na kiuchumi na Ethiopia na Eritrea.

Ramani ya Somalia

Kwa mujibu wa Katiba ya Somalia, Wabunge wapatao 92 wanapaswa kusaini hoja hiyo ya kutokuwa na imani na Rais, ili Spika aruhusu kuanza kwa mjadala huo bungeni.

Mapema Jumatatu wafuasi wa Rais Farmajo wa Somalia walifanya maandamano katika mji mkuu Mogadishu, kupinga kitendo hicho cha wabunge kuwasilisha hoja bungeni ya kutaka kupiga kura ya kutokuwa na imani na rais huyo.