Wasudan 8 wauawa katika machafuko ya kupinga hali mbaya ya uchumi
Wasudan wasiopungua 8 wameuawa katika ghasia na maandamano ya wananchi ya kupinga hali mbaya ya kiuchumi, ughali wa bidhaa na maisha magumu nchini humo.
Maafisa wa serikali ya Sudan wametangaza usiku wa kuamkia leo kwamba, idadi ya watu waliouawa katika maandamano ya kupinga hali mbaya ya kiuchumi katika mikoa ya al Qadharif na Nahru Nil imefikia 8.
Tangu Jumatano ya juzi miji mbalimbali ya Sudan ilishuhudia ghasia na maandamano makubwa ya wananchi wanaopinga hali mbaya ya kiuchumi na ughali wa bidhaa.
Maafisa wa serikali katika baadhi ya mikoa ya nchi hiyo kama Al Qadarif wamelazimika kutangaza hali ya hatari baada ya kuuliwa waandamanaji 5. Ghasia na maandamano ya kupinga hali mbaya ya uchumi na ughali wa maisha na bidhaa yaliyoanzia katika miji ya Atbara na Port sasa yameingia katika mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum.
Waandamanaji hao pia wamechoma moto majengo ya serikali na vituo vya chama tawala cha Kongresi ya Taifa.
Waandamanaji hao ambao wanalalamikia kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu kama mkate na hali mbaya ya uchumi wanataka kuondolewa madarakani serikali ya Sudan.