Mtu mwingine auawa katika ghasia Sudan, Khartoum yasema Israel inachochea machafuko
Mkuu wa taasisi ya upelelezi ya Sudan amesema kuwa waasi wenye uhusiano na utawala haramu wa Israel ndio wanaochochea maandamano yanayoendelea kwa siku kadhaa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo ambayo yamesababisha kifo cha mtu mmoja jana baada ya mauaji ya waandamanaji wengine wasiopungua 8 siku kadhaa zilizopita.
Salah Abdallah Gosh amesema mtandao wenye makao yake katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi ambao una uhusiano na Israel umeingiza mamia ya waasi nchini Sudan kwa shabaha ya kuchochea machafuko nchini humo.
Mkuu wa vyombo vya upelelezi vya Sudan amesema kuwa vyombo vya usalama vimewatia nguvuni watu kadhaa ambao ni sehemu ya wafuasi 280 wa kundi la waasi la Abdul Wahid Mohamed Nur walioingizwa Sudan kupitia Nairobi.
Gosh ameongeza kuwa watu hao wameajiriwa na shirika la ujasusi la Israel, Mossad na wamefungua ofisi za kuendeshea operesheni zao katika miji ya Kharoutm na Omdurman. Ameongeza kuwa vyombo vya usalama pia vimewatia nguvuni watu kadhaa waliohusika na machafuko ya siku kadhaa zilizopita katika mji wa Atbara.
Vyuo vikuu na taasisi za elimu zimefungwa nchini Sudan na serikali imetangaza hali ya hatari katika miji kadhaa ya nchi hiyo kutokana na maandamano yanayoendelea kupinga hali mbaya ya uchumi na ughali wa bidhaa.
Waandamanaji hao pia wamechoma moto majengo ya serikali na vituo vya chama tawala cha Kongresi ya Taifa.
Waandamanaji hao ambao wanalalamikia kupanda kwa bei ya bidhaa muhimu kama mkate na hali mbaya ya uchumi wanataka kuondolewa madarakani serikali ya Sudan.