Jeshi la Sudan laamrishwa kuingilia kati, serikali yaapa kukabiliana na machafuko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50364-jeshi_la_sudan_laamrishwa_kuingilia_kati_serikali_yaapa_kukabiliana_na_machafuko
Jeshi la Sudan limetakiwa kuingia uwanjani kwa ajili ya kukabiliana na maandamano yanayopinga serikali ya Rais Omar al Bashir yanayoendelea kwa siku kadhaa sasa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Dec 23, 2018 08:38 UTC
  • Jeshi la Sudan laamrishwa kuingilia kati, serikali yaapa kukabiliana na machafuko

Jeshi la Sudan limetakiwa kuingia uwanjani kwa ajili ya kukabiliana na maandamano yanayopinga serikali ya Rais Omar al Bashir yanayoendelea kwa siku kadhaa sasa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo.

Makamu wa Rais wa Sudan, Faisal Hassan Ibrahim amesema Kamati ya Usalama wa Taifa imeliamuru jeshi kulinda maeneo ya kistratijia ya mali za umma na kwamba polisi na kikosi cha usalama kitakabiliana na waandamanaji. 

Hassan Ibrahim ameongeza kuwa, mgogoro wa sasa wa kiuchumi wa Sudan unahitajia muda na kwamba vuruga na mchafuko havikubaliwi. 

Hatua hiyo ya kuliamuru jeshi kukabiliana na waandamanaji nchini Sudan imechukuliwa baada ya kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Sadiq al-Mahdi kutangaza kuwa raia wasiopungua 22 wameuawa hadi sasa katika maandamano ya wananchi yanayolalamikia hali mbaya ya uchumi na kupanda kwa gharama za maisha. 

Sadiq al-Mahdi

Sadiq al-Mahdi ametoa wito wa kuundwa serikali mpya itakayoiepusha Sudan na athari mbaya za machafuko na mapinduzi kama yale yaliyozikumba nchi kadhaa za Kiarabu miaka kadhaa iloyopita. Vilevile ameitaka serikali kukomesha ukandamizaji na kushughulikia matakwa ya wananchi la sivyo itakabiliwa na ghadhabu zao.

Wakati huohuo, wanachama 14 wa muungano wa upinzani wa National Consensus Forces wametiwa mbaroni wakituhumiwa kuchochea maandamano hayo.

Serikali ya Khartoum inasisitiza kuwa, mtandao wenye makao yake katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi ambao una uhusiano na Israel umeingiza mamia ya waasi nchini Sudan kwa shabaha ya kuchochea machafuko nchini humo.