Maandamano Sudan, sababu na mustakabali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50365-maandamano_sudan_sababu_na_mustakabali
Katika siku za hivi karibuni wananchi wa Sudan wamejitokeza mitaani na kuandamana kutokana na ughali wa mkate nchini humo na sasa malengo ya maandamano hayo yamebadilika na kuwa ya matakwa jumla ya mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 23, 2018 08:52 UTC
  • Maandamano Sudan, sababu na mustakabali

Katika siku za hivi karibuni wananchi wa Sudan wamejitokeza mitaani na kuandamana kutokana na ughali wa mkate nchini humo na sasa malengo ya maandamano hayo yamebadilika na kuwa ya matakwa jumla ya mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa.

Maandamano hayo yalianza Jumatano katika mji wa Atbara kaskazini mashariki mwa Sudan kutokana na ughali na uhaba wa mkate ambacho ni chakula cha kila siku cha wakazi wa nchi hiyo. Maandamano hayo ambayo yalianza kutokana na sababu za kiuchumi sasa yameenea katika miji mingine ya Sudan na kuwa matakwa ya mabadiliko ya kisiasa. Vikosi vya usalama vimetumia nguvu ziada kukabiliana na waandamanaji na hadi kufikia Jumapili hii watu 22 walikuwa wameshauawa.

Kwa muda wa miaka kadhaa sasa Sudan imekuwa ikikumbwa na matatizo makubwa ya kiuchumi. Baada ya kujitenga Sudan Kusini, eneo lenye utajiri wa mafuta, Sudan ilipoteza asilimia 60 ya pato  la mafuta ambalo ilikuwa ikilipata kutoka eneo hilo. Matatizo mengine ya serikali ya Sudan ni ukosefu wa ajira, umasikini, ufisadi na ubadhirifu wa fedha za umma.

Rais Omar al Bashir wa Sudan

Ingawa maandamano hayo msingi wake ni matatizo makubwa ya kiuchumi na ughali wa maisha nchini Sudan, lakini sasa wananchi wameanza kutoa matakwa ya kisiasa ambayo yanapaswa kuzingatiwa.

Maandamano nchini Sudan yalianza wakati waziri mkuu wa zamani wa Sudan, Sadeq al Mahdi ambaye ni Mwenyekiti wa muungano wa "Nedaa Sudan" na mpinzani mkali wa Rais Omar al Bashir, aliporejea Khartoum wiki iliyopita ambapo aliwataka wafuasi wake waanzishe  harakati za mabadiliko ya kidemokrasia na kuchukua madaraka kwa amani.

Katika miezi ya hivi karibuni serikali ya Sudan na wafuasi wa Omar al Bashir wamekuwa wakijaribu kubadilisha katiba ya nchi hiyo ili kumwandalia mazingira ya kuendelea kubakia madarakani.

Akigusia suala hilo kwa njia isiyo ya moja kwa moja Sadeq al Mahdi amesema: "Uchaguzi ndio njia bora zaidi ya utawala lakini tunapaswa kuwa na tume huru ya uchaguzi ambayo itaweza kusimamia uchaguzi kwa mujibu wa sheria."

Kushiriki Sudan katika muungano wa Saudia dhidi ya watu wa Yemen ni suala lingine ambao limewakasirisha sana wananchi wa Sudan. Omar al Bashir alijiunga na muungano wa vita dhidi ya Yemen ili apokee msaada wa kifedha kutoka Saudia na ili kuboresha uhusiano wa nchi yake na Marekani sambamba na kueondolewa vikwazo vya kisiasa na kichumi ambavyo Washington ilikuwa imeweka dhidi ya Khartoum.

Viongozi wengi wa kisiasa nchini Sudan wanaamini kuwa, kushiriki katika muungano wa vita dhidi ya Yemen kumeisababishia nchi yao hasara kubwa, mbali na kuwa uamuzi huo pia umekiuka sera za Sudan za kutopendelea upande wowote.

Kiongozi wa upinzani Sudan, Sadeq al Mahdi

Abdulbari Atwan, mwandishi habari Mwarabu anasema Rais al-Bashir amegonga mwamba katika mahesabu yake. Anasema" Wakati al-Bashir alipojiunga na muungano wa kivita wa Saudia na Imarati dhidi ya Yemen alikuwa anataka vikwazo vya kisiasa na kiuchumi alivyokuwa amewekewa na Marekani viondolewe na pia alilenga kupokea msaada wa mabilioni ya fedha kutoka Saudia na Imarati na kujikwamua kwenye matatizo ya kiuchumi, lakini sasa hajafikia malengo yote hayo.

Omar al Bashir amekuwa akibadilisha misimamo yake mara kwa mara katika masuala yanayohusu nchi za Kiarabu, Kiafrika na hata za Magharibi ili kubakia madarakani. Lakini sasa anakabiliwa na hasira za wananchi ambao kilio chao kikubwa ni kuongezeka bei ya mkate, na katika upande wa pili waitifaki wake aliowategemea wamemuacha mkono. Hayo yanajiri huku uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya Sudan ukizidisha hali mbaya nchini humo.

Katika hali kama hii inaelekea kuwa, Rais al Bashir hatakuwa na budi ila kusikiliza matakwa ya wananchi au aendelee kukandamiza maandamano kwa mkono wa chuma, suala ambayo yamkini likaishia kwa utawala wake kuondolewa madarakani.