Maandamano ya wapinzani yaendelea nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50382-maandamano_ya_wapinzani_yaendelea_nchini_sudan
Wananchi wa Sudan wanaendelea na maandamano yao ya kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi nchini mwao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 24, 2018 04:32 UTC
  • Maandamano ya wapinzani yaendelea nchini Sudan

Wananchi wa Sudan wanaendelea na maandamano yao ya kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi nchini mwao.

Mapema leo alfajiri, shirika la habari la IRNA limeripoti kuwa, jana usiku polisi wa Sudan walitumia mabomu ya kutoa macho kuwatawanya waandamanaji katika mji mkuu wa nchi hiyo, Khartoum.

Waandamanaji hao walipiga nara za kuipinga serikali na kutaka kutatuliwa matatizo yao mengi ya kiuchumi na wanataka serikali ya Rais Omar al Bashir iondolewe madarakani kwa kushindwa kuendesha nchi.

Rais Omar al Bashir wa Sudan

 

Tangu Jumatano iliyopita hadi hivi sasa miji mbalimbali ya Sudan inashuhudia maandamano ya kulalamikia hali mbaya ya kiuchumi na kupanda kwa bei za bidhaa hasa mikate na mafuta.

Serikali ya Sudan imetangaza hali ya hatari na amri ya kutotoka nje katika baadhi ya mikoa sambamba na kufunga mashule na vyuo vikuu vikiwemo vya mjini Khartoum.

Serikali inadai kuwa watu 8 wameshauawa hadi hivi sasa kwenye maandamano hayo lakini duru za kujitegemea na zisizo za serikali zinasema kuwa waliouawa hadi hivi sasa ni baina ya watu 22 hadi 28 huku makumi ya wengine wakijeruhiwa.