Dec 28, 2018 03:02 UTC
  • Baraza la Dini Ethiopia lakutana na viongozi wa OLF

Baraza la Dini la Ethiopia pamoja na makundi ya wazee jana Alkhamisi yalikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa kundi la wabeba silaha la Harakati ya Ukombozi ya Oromo (OLF).

Mkutano huo umefanyika kwa lengo la kuhitimisha mgogoro na mapigano ya mara kwa mara katika jimbo la Oromia. Viongozi hao wa kidini wametoa mwito kwa vyama siasa kuitafutia ufumbuzi migogoro iliyopo ili kuhitimisha mauaji na watu kufurushwa makwao katika jimbo hilo.

Wiki jana viongozi hao wa kidini walikutana na Lemma Megersa, Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia cha Oromo ODP na Ofisa Mkuu wa jimbo la Oromia.

Wakazi wa Oromia wakifanya maanadamano

Kundi la Harakati ya Ukombozi ya Oromo linakadiriwa kuwa na wapiganaji 2,800 wakiwa sehemu ya magharibi ya jimbo la Oromia, katika miezi ya hivi karibuni limekuwa likifanya mashambulizi dhidi ya jeshi na raia.

Hivi karibuni watu 23 waliuawa katika machafuko yaliyozuka jirani na mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa, baada ya wafuasi wa kundi la zamani la waasi la Harakati ya Ukombozi wa Oromo (OLF) ambao wengi wao wanatoka katika kabila la Oromo, kuingia mjini Addis Ababa wakipeperusha bendera ya OLF na kupambana na wakazi wa mji huo.

Tags