Al Bashir aamuru kuundwe tume ya kuchunguza machafuko ya sasa nchini Sudan
Rais Omar al Bashir wa Sudan ametoa amri ya kuundwa tume ya kuchunguza ghasia na machafuko yanayoendelea sasa nchini humo.
Habari hiyo imetangazwa na shirika la habari la Sudan, SUNA bila ya kutoa maelezo zaidi na kwamba Waziri wa Sheria wa nchi hiyo, Mohamed Ahmed Salem ndiye atakayeongoza tume hiyo.
Jeshi la Polisi la Sudan limetangaza kuwa hali ya utulivu imeanza kurejea katika majimbo mbalimbali ya nchi hiyo isipokuwa majimbo mawili ya Khartoum na Sennar huko kusini mashariki mwa Sudan.
Katika upande mwingine chama cha Umma kimetangaza kuwa, askari usalama wa nchi hiyo wamemtia nguvuni Zainab Sadiq al Mahdi, binti wa kiongozi wa chama hicho cha upinzani, Sadiq al Mahdi.
Wananchi wa Sudan wamekuwa wakifanya maandamano katika majimbo karibu yote ya nchi hiyo wakilalamikia hali mbaya ya uchumi na ughali wa bidhaa. Maandamano hayo yaliyopewa jina la "Maandamano ya Mkate" sasa yamechukua mkondo mpya na waandamanaji wanataka kuondolewa madarakani serikali ya Rais Omar al Bashir.
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeripoti kuwa, watu wasiopungua 38 wameuliwa hadi sasa katika machafuko hayo.