Kuendelea maandamano ya kupinga serikali nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i50736-kuendelea_maandamano_ya_kupinga_serikali_nchini_sudan
Katika hali ambayo malalamiko na maandamano dhidi ya serikali yanaendelea nchini Sudan, Rais Omar Hassan al-Bashir wa nchi hiyo ameanza safari ya kutembelea baadhi ya majimbo ya nchi hiyo kwa shabaha ya kutuliza hali ya mambo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 08, 2019 21:28 UTC
  • Kuendelea maandamano ya kupinga serikali nchini Sudan

Katika hali ambayo malalamiko na maandamano dhidi ya serikali yanaendelea nchini Sudan, Rais Omar Hassan al-Bashir wa nchi hiyo ameanza safari ya kutembelea baadhi ya majimbo ya nchi hiyo kwa shabaha ya kutuliza hali ya mambo.

Malalamiko na maandamano dhidi ya serikali yalianza Disemba 19 kupinga ongezeko la bei ya mkate na nishati ya mafuta na yakasambaa katika miji mbalimbali ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa takwimu za serikali hadi sasa watu 19 wameuawa na makumi ya wengine wametiwa mbaroni. Hali mbaya ya uchumi, kuporomoka kiwango cha maisha na kuongezeka umasikini na ukosefu wa ajira ni mambo ambayo yamelipua ghadhabu za wananchi wa Sudan na kuwafanya waanzishe maandamano na malalamiko dhidi ya hali mbaya ya kiuchumi na sera za Rais Omar Hassan al-Bashir katika uga wa siasa na kiuchumi.

Kadhalika kuendelea vita vya ndani, kujitenga Sudan Kusini, kupungua nafasi ya Sudan ya kufikia vyanzo vya utajiri wa mafuta, kuongezeka ufisadi wa kifedha na kushiriki vikosi vya nchi hiyo katika vita vya Yemen vya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ni mambo ambayo yameshadidisha matatizo ya Sudan.

Rais Omar Hassan al-Bashir

Licha ya kuwa waandamanji awali walimiminika mabarabarani wakilalamikia hali mbaya ya uchumi, lakini hivi sasa maandamano yao yamechukuua mkondo wa kisiasa, ambapo waandamanaji wanataka Rais Omar al-Bashir aondoke madarakani na kuandaliwa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru na katika anga salama na ya amani. 

Chama cha "Nidaa al-Sudan" kinachohesabiwa kuwa moja ya vyama muhimu vya upinzani nchini Sudan Januari Pili mwaka huu, kilitoa taarifa rasmi kikitaka Rais Omar al-Bashir aachie ngazi na kuandaliwa mazingira ya kidemokrasia katika nchi hiyo kupitia mchakato wa ubadilishanaji madaraka.

Kutokuweko uhuru wa kisiasa na kijamii, kukandamizwa waandamanaji, kupuuzwa matakwa ya wananchi na siasa za kidikteta za Rais al-Bashir ni miongoni mwa mambo ambayo yameshadidisha hasira za waandamanaji nchini Sudan. Katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, viongozi wa Sudan wamefanya harakati mbalimbali zenye lengo la kubadilisha katiba ya nchi hiyo na kumuandalia uwanja Omar al-Bashir wa kuwania tena kiti cha urais katika uchaguzi ujao. Hili ni jambo ambalo, nalo pia limechochea malalamiko na radiamali za akthari ya wanasiasa na wanaharakati wa masuala ya kiraia nchini Sudan.

Sadeq al-Mahdi, mmoja wa viongozi muhimu wa upinzani nchini Sudan

Majimui ya matatizo haya, kwa sasa yameitumbukiza Sudan katika dimbwi kubwa la malalamiko ya kijamii na kisiasa, kiasi kwamba, kuendelea na kuchukua wigo mpana malalamiko haya, kumemlazimisha Rais al-Bashir, mbali na kulifanyia mabadiliko baraza lake la mawaziri, aahidi pia kuboresha hali ya maisha ya wananchi sambamba na kutekeleza matakwa yao.

Kuhusiana na hili, Rais Omar al-Bashir ameanzia safari yake ya ndani huko katika jimbo la Mto Nile mahala yalipoanzia malalamiko. Rais al-Bashir ameahidi pia kuongeza mishahara ya wafanyakazi wa serikkali, kuongeza marupurupu ya bima ya tiba na mishahara ya wastaafu huku akiwataka wapinzani wake kushiriki katika uchaguzi ujao.

Akizungumza mjini Khartoum tarehe 6 ya mwezi huu wa Januari, Rais wa Sudan alisema kuwa, watu ambao wanataka yeye aachie ngazi na kuondoka madarakani wajiandae kushiriki katika uchaguzi ujao hapo mwakani 2020 na kuchukua hatamu za uongozi wa nchi. Aidha Rais wa Sudan aliahidi kuandaa mazingira mazuri kwa ajili ya wananchi wa nchi hiyo na kuleta usalama wa nchi.

Maandamano ya wananchi ya kulalamikia kupanda gharama za maisha

Rais wa Sudan anachukua hatua hizo katika hali ambayo, malalamikko na maandamano ya wananchi yameingia katika wiki yake ya tatu huku jumuiya, vyama vya upinzani, waajiri na wasomi wa vyuo vikuu wakitoa miito kwa wananchi kushiriki katika maandamano dhidi ya serikali.

Katika mazingira kama haya, inaonekana kuwa, kuna haja ya kusubiri kuona taathira za ahadi na mipango ya Rais al-Bashir kwa ajili ya kutuliza ghadhabu na hasira za waandamanaji; pamoja na kuwa haionekani kama ahadi zake hizo zinaweza kupunguza wigo wa malalamiko hayo.