Mafuriko yaua watu wawili Tanzania
Watu wawili wamethibitishwa kufariki dunia na mamia ya wengine kuachwa bila makao baada ya mvua kubwa kunyesha kwa wiki moja katika wilaya ya Kyela, kusini magharibi mwa Tanzania.
Mkuu wa wilaya ya Kyela Thea Ntara amesema nyumba na barabara zimeharibiwa na kufanya huduma za jamii ikiwa ni pamoja na shule kufungwa katika wilaya hiyo inayopakana na Malawi. Amesema kwa sasa bado wanaendelea kukusanya taarifa, na idadi ya watu waliofariki inaweza kuongezeka kutokana na baadhi ya maeneo kutofikika. Pia amesema kwenye baadhi ya maneno waliyofikia, wahanga wanahitaji msaada wa chakula, dawa, pamoja na maji safi na salama.
Huku hayo yakiripotiwa, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kunyesha mvua kubwa inayozidi milimita 50 wiki hii. Imesema mvua hizo ambazo zitanyesha katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba zitakuwa kubwa na kuweza kusababisha madhara.
Wiki hii mvua zilizonyesha katika jiji la Dar es Salaam zimesababisha mafuriko katika maeneo ya katikati ya jiji na kusababisha baadhi ya maduka kufungwa na magari kuzimika barabarani kutokana na kuingiwa na maji kulikotokana na tatizo sugu la miundombunu ya maji taka.
Wakazi wa jiji la Dar es Salaam wameitaka serikali kutenga fedha na kuweka mikakati maalumu ili kuondoa kero sugu ya tatizo la miundombinu ya maji taka katika jiji hilo.