Wasiwasi wa UN kuhusu kuuawa waandamanaji Sudan
Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet amesema ana wasiwasi mkubwa juu ya ghasia zinazoendela nchini Sudan ambazo hadi sasa zimesababisha kuuawa kwa watu 24 na wengine wengi kujeruhiwa.
Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu iliyotolewa Alhamisi mjini Geneva, Uswisi inasema kuwa kuna taarifa za uhakika ya kwamba vikosi vya usalama vinatumia nguvu kupita kiasi ikiwemo silaha za moto dhidi ya waandamanaji, hali ambayo inatia wasiwasi mkubwa.
Akihojiwa mjini Geneva, Uswisi, msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Ravina Shamdasani amesema, “vikosi vya usalama vinawafuata waandamanaji hadi hospitali ya Omdurman na kufyatua risasi pamoja na mabomu ya kutoa machozi. Hii kwa hakika haikubaliki, tunatoa wito kwa mamlaka zihakikishe kuwa haki ya watu kukusanyika na kuandamana kwa amani inalindwa bila kujali mirengo yao ya kisiasa.”
Msemaji huyo amemnukuu Kamishna Bachelet akisema kuwa, "kuna malalamiko ya kweli lakini si kwamba tunasema ni rahisi kuyapatia majibu. Lakini jawabu kandamizi linaweza kufanya malalamiko hayo kuwa mabaya zaidi.”
Wakati serikali ya Sudan ikidai kuwa ni watu 24 waliouawa hadi hivi sasa, shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limesema kuwa, watu wasiopungua 40 wameshauawa katika maandamano hayo yaliyoanza tarehe 19 Disemba 2018, wakiwemo watoto wadogo na maafisa wa kutoa misaada.
Uchumi wa Sudan umekumbwa na mgogoro kutokana na kukosekana fedha za kutosha za kigeni na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu. Thamani ya sarafu ya nchi hiyo nayo imeporomoka. Waandamanaji sasa mbali na kutaka hali ya uchumi iboreke wanataka Rais Omar al Bashir aondoke madarakani.