Wahandisi wajiunga na maandamano ya wapinzani nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51092-wahandisi_wajiunga_na_maandamano_ya_wapinzani_nchini_sudan
Kundi la wahandishi wa Sudan limejiunga na maandamano ya kupinga serikali ya nchi hiyo katika mji mkuu Khartoum.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Jan 24, 2019 12:26 UTC
  • Wahandisi wajiunga na maandamano ya wapinzani nchini Sudan

Kundi la wahandishi wa Sudan limejiunga na maandamano ya kupinga serikali ya nchi hiyo katika mji mkuu Khartoum.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, wahandisi wa Sudan leo Alkhamisi wameandamana mbele ya majengo ya chama cha wahandisi wakiwa wamebeba beramu linalomtaka Rais Omar al Bashir ang'oke madarakani. Walioshiriki kwenye maandamano hayo wamesema kuwa, hawawatambui viongozi wa chama cha wahandisi wa nchi hiyo kwani ni wafuasi wa Omar al Bashir.

Duru za Sudan zimetangaza kuwa, askari wa serikali wametumia nguvu kama vile vifaa vya kusisimua mwili kwa kutumia umeme na mabomu ya kutoa machozi sambamba na kuwatia mbaroni wahandisi waliofanya maandamano hayo.

Waandamanaji wanamtaka Rais Omar al Bashir ang'oke madarakani 

 

Sudan imekumbwa na maandamano tangu tarehe 19 Disemba mwaka jana, ambapo malalamiko makubwa ya wananchi wanaoandamana ni ughali wa maisha na kupanda bei za bidhaa muhimu hasa mkate na mafuta. Viongozi wa nchi hiyo wanadai kuwa hadi sasa watu 24 wameshauawa kwenye maandamano hayo.

Hata hivyo shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International kwa kutegemea ripoti za kuaminika limesema kuwa, hadi sasa watu 40 wameshauawa kwenye maandamano hayo.

Maandamano hayo ni makubwa zaidi kuwahi kuikumba Sudan katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Sasa waandamanaji wanataka Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo ang'oke madarakani, lakini bado anashikilia msimamo wake wa kubakia uongozini. Serikali ya Sudan imetangaza hali ya hatari katika baadhi ya mikoa ya nchi hiyo sambamba na kufunga shule na vyuo vikuu.

Omar al Bashir yuko madarakani nchini Sudan tangu mwaka 1993 ambapo kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, muda wa mwisho wa kubakia kwake madarakani ni mwakani yaani 2020.