Al Bashir: Utawala haubadilishwi kwa WhatsApp na Facebook
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i51256-al_bashir_utawala_haubadilishwi_kwa_whatsapp_na_facebook
Rais Omar al Bashir wa Sudan amekemea maandamano yanayoendelea kufanywa na wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo dhidi ya serikali yake na kusema kuwa utawala hauwezi kubadilishwa kwa kutumia njia kama za WhatsApp na Facebook bali kupitia madanduku ya kupigia kura.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 01, 2019 03:59 UTC
  • Rais Omar al Bashir wa Sudan
    Rais Omar al Bashir wa Sudan

Rais Omar al Bashir wa Sudan amekemea maandamano yanayoendelea kufanywa na wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo dhidi ya serikali yake na kusema kuwa utawala hauwezi kubadilishwa kwa kutumia njia kama za WhatsApp na Facebook bali kupitia madanduku ya kupigia kura.

Matamshi hayo ya al Bashir yametolewa huku Wasudani wakiendeleza maandamano makubwa dhidi ya utawala wake katika miji mbalimbali ya nchi hiyo. 

Omar al Bashir ambaye alikuwa akihutubia wafuasi wake katika mji wa Kassala huko mashariki mwa Sudan amesema kuwa tawala na viongozi hawawezi kubadilishwa kwa kutumia WhatsApp na Facebook bali kupitia uchaguzi na kwamba taifa la Sudan ndilo litakaloainisha nani atatawala nchi yao.

Wakati huo huo vitongoji mbalimbali vya jiji la Khartoum jana vilishuhudia maandamano makubwa yaliyoitishwa na kambi ya upinzani yaliyopewa jina la msafara mkubwa wa kuelekea Ikulu. Maandamano mengine kama hayo yameshuhudiwa katika miji na maeneo mengine ya Sudan licha ya polisi na askari usalama kukabiliana na waandamanaji kwa kutumia gesi ya kutoa machozi.

Wasudan wanaandamana kupinga serikali ya al Bashir

Katika upande mwingine Mkuu wa Usalama wa taifa wa Sudan Salah Abdallah Gosh amesema jeshi la nchi hiyo liko tayari kuelekea Khartoum kuzima machafuko na kudai kuwa baadhi ya wanaosimamia maandamano hayo wana mfungamano na nchi za kigeni. 

Ni wiki kadhaa sasa Sudan imegubikwa na maandamano na ghasia huku wafanya maandamano wakisisitiza kuwa utawala wa miongo mitatu wa Rais Omar al Bashir unapasa ufikie kikomo. Maandamano nchini Sudan awali yalichochewa na hatua ya serikali ya kupandisha mara tatu bei ya mkate; hatua iliyochochea moto wa maandamano dhidi ya serikali karibu katika miji yote ya nchi hiyo.