Feb 09, 2019 07:44 UTC
  • Watu wengine 7 wauawa katika hujuma ya kigaidi nchini Msumbiji

Kwa akali watu saba wameuawa katika shambulizi jingine la kigaidi huko kaskazini mwa Msumbiji.

Mwanachama wa Baraza la Wazee ambaye hakutaka kutaja jina lake ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, magaidi hao waliua wanaume saba na kukatakata miili yao vipande vipande, na kisha kuvitupa katika kijiji cha Piqueue.

Ameongeza kuwa, mbali na mauaji hayo ya kinyama, lakini pia wanachama hao wa genge la ukufurishaji wamewateka nyara wanawake wanne katika uvamizi huo wa usiku wa kuamkia jana.

Polisi ya Msumbiji imekataa kutoa taarifa yoyote kuhusu mauaji hayo mapya ya kigaidi, lakini kamanda mmoja wa jeshi katika eneo hilo amethibitisha habari ya kutokea shambulizi hilo.

Vijiji vya mkoa huo wa Cabo Delgado ulioko kaskazini mwa Msumbiji tangu mwezi Oktoba mwaka 2017 vimekuwa vikishuhudia mashambulizi ya umwagaji damu ya wanachama wa kundi linalojiita Ahlu Sunna Wal Jamaa, ambao wakazi wa maeneo hayo wanawatambua kwa jina la al-Shaabab.

Maafisa usalama wakishika doria katika mkoa wa Cabo Delgado

Mwezi uliopita wa Januari, abiriwa 12 waliuawa baada ya basi lao kumiminiwa risasi na genge la kitakfiri katika mji wa Manilha mkoani Cabo Delgado, kaskazini mwa nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.

Baada ya kushadidi hujuma hizo, serikali ya Msumbiji ilituma wanajeshi na polisi katika maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Tanzania na tayari mamia ya washukiwa wamekamatwa.

Tags