Sadiq al Mahdi amuonya Rais al Bashir asiendelee kukandamiza waandamanaji Sudan
-
Sadiq al Mahdi, kiongozi wa chama cha Umma cha Sudan
Kiongozi wa kambi ya upinzani nchini Sudan ameionya serikali ya Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo kuhusiana na hatari ya kuendelea kukandamizwa wananchi wanaoandamana kwa amani.
Sadiq al Mahdi, kiongozi wa chama cha Umma cha Sudan ambaye ni mpinzani mkuu wa serikali ya nchi hiyo amesema, huu ndio wakati wa mabadiliko kwani maandamano ya wananchi nchini Sudan yametokana na kurundikana matatizo mengi juu yao.
Ameongeza kuwa, misikiti ina nafasi kubwa katika kuleta umoja na mshikamano wa wananchi na kufichua ukandamizaji wa serikali ya Sudan.
Sudan imekumbwa na maandamano tangu katikati ya mwezi Disemba 2018 na chanzo cha maandamano hayo kilikuwa ni kulalamikia kupanda bei za bidhaa muhimu hasa mkate na mafuta.
Maandamano hayo yameenea nchi nzima na sasa waandamanaji wanataka Rais Omar al Bashir aong'oke madarakani baada ya kuitawala nchi hiyo kwa takriban miaka 30 sasa, yaani tangu tarehe 30 Juni 1989.
Maandamano ya hivi sasa hayajawahi kutokea mfano wake nchini Sudan katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita.
Kwa mujibu wa shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International, makumi ya watu wameshauawa na kujeruhiwa kutokana na ukandamizaji wa vikosi vya serikali ya nchi hiyo.