Mabadiliko makubwa nchini Sudan katika kivuli cha mgogoro wa kisiasa
-
Rais Omar al Bashir wa Sudan
Rais Omar al Bashir wa Sudan katika hatua ambayo haikutazamiwa amevunja baraza la mawaziri la serikali yake na kutangaza hali ya hatari katika maeneo yote nchini humo. Hatua hiyo imechukuliwa huku Sudan ikiendelea kuzongwa na maandamano yanayomtaka kiongozi huyo ang'atuke madarakani.
Mgogoro wa Sudan ulianza Disemba 19 mwaka jana baada ya wananchi kuanza kuandamana wakilalamikia hali ngumu ya kiuchumi na kupanda bei za bidhaa mbalimbali hususan bei ya mkate na petroli. Mgogoro huo uliopanuka zaidi na kushika mkondo wa kisiasa na kiuchumi baada ya askari usalama kuingilia kati na kukandamiza wananchi wanaoandamana na kujitokeza vyama vya kisiasa na kuunga mkono maandamano hayo ya upinzani.
Kwa muda sasa Sudan inasumbuliwa na hali mbaya ya kiuchumi. Hatua ya Sudan Kusini ya kujitenga na Sudan na kuifanya nchi hiyo ipoteze sehemu kubwa ya akiba yake ya mafuta, kuwepo ufisadi na ubadhirifu mkubwa wa fedha za umma, kuendelea vita vya ndani katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, siasa mbovu za Omar al Bashir na hatua ya Sudan ya kuiunga mkono Saudia katika vita vyake huko Yemen na kuongezeka gharama za kijeshi, yote hayo yamezidisha matatizo ya kiuchumi ya Sudan. Hali hiyo imezidisha umaskini, ukosefu wa ajira, uhaba wa bidhaa za chakula na kupanda sana kwa bei za bidhaa muhimu kama mkate na mwishowe kuzidisha hasira na ghazabu za raia wa Sudan.
Katika upande mwingine, kukandamizwa wapinzani wa serikali, kukosekana uhuru wa kiraia na jitihada za Rais al Bashir za kutaka kuifanyia marekebisho katiba kwa lengo la kuandaa mazingira ya kugombea tena kiti cha rais wa Sudan vimechochea zaidi maandamano dhidi ya serikali. Wafanya maandamano wanamtaka Rais al Bashir ang'atuke madarakani na kuitishwe uchaguzi huru na wa amani huko Sudan.
Harakati ya Kitaifa ya Mabadiliko ya Sudan inayoundwa na vyama 22 vya upinzani kikiwemo chama cha Umma kinachoongozwa na Sadiq al Mahdi, imesaini taarifa ya pamoja na kumtaka Rais Omar al Bashir avunje Serikali na Bunge na kuunda baraza la mpito kwa ajili ya kusimamia masuala ya nchi ili Khartoum iweze kuondokana na mgogoro wa sasa.
Upinzani Sudan umewasilisha matakwa yake hayo huku askari usalama wakiendelea kuyakandamiza maandamano ya wananchi na hadi sasa makumi ya waandamanaji wakiwemo viongozi wa vyama na waandishi habari wameuawa au kutiwa nguvuni.
Sadiq al Mahdi kiongozi wa chama cha upinzani cha Umma ametahadharisha kuhusu ukandamizaji unaoendelea kufanywa na serikali dhidi ya wananchi wanaoandamana nchini Sudan na kusisitiza kuwa: Umewadia wakati wa kufanyika mageuzi kwa sababu kuendelea maandamano ya wananchi ni matokeo ya kushtadi matatizo mbalimbali nchini Sudan.
Mwanzoni mwa mgogoro wa ndani wa Sudan Omar al Bashir alizituhumu nchi za Magharibi kuwa zina mkono katika kuchochea maandamano na mgogoro huo na kusema mgogoro wa kiuchumi nchini humo unasababishwa na vikwazo vya nchi za Magharibi dhidi ya nchi hiyo. Baada ya kupanuka mgogoro huo Rais al Bashir ameahidi kuboresha hali ya mambo nchini na ameyatolea wito makundi ya upinzani kuketi kwenye meza ya mazungumzo ya kitaifa, suala ambalo limepingwa na wapinzani.
Kutokana na kuendelea hali hiyo ya mgogoro, Rais Omar al Bashir ameamua kutangaza hali ya hatari kote nchini Sudan, kuvunja serikali na kuwafuta kazi magavana wa majimbo yote 18 nchini humo. Badala yake al Bashir amewateuwa maafisa usalama wakiwemo wanajeshi kujaza nafasi za magavana hao. Japokuwa imeelezwa kuwa, al Bashir amechukua hatua hiyo ili kupambana na ufisadi na kujaribu kurekebisha hali ya mambo, lakini watu wengi wana wasiwasi kuhusu uwezekano wa kuongezeka ukandamizaji na kuuliwa waandamanaji katika siku zijazo.
Hali ya mambo nchini Sudan imezidi kuwa mbaya huku wafanya maandamano wakiwemo wapinzani wakitangaza kuwa hawatanyamaza kimya hadi hapo matakwa yao yatakapopatiwa ufumbuzi. Katika upande wa pili pia serikali ya Khartoum inajaribu kutumia nyenzo zote kutuliza hali ya mambo. Hali hii inaashiria kuwa, Sudan inapitia moja ya vipindi vigumu katika historia yake ya kisiasa.