Wasudan wafanya mgomo kumshinikiza Rais Bashir ajiuzulu
Mgomo wa siku moja uliotishwa hii leo kwa ajili ya kumshinikiza Rais Omar al-Bashir wa Sudan aachie ngazi umelemaza shughuli za kila siku katika mji mkuu wa nchi hiyo Khartoum.
Maduka mengi na masoko yamesalia kufungwa hii leo katika mji huo, huku barabara zikikosa pilikapilika za kila siku kutokana na mgomo huo.
Maelfu ya wafanyakazi hususan wa sekta za umma wameshiriki mgomo huo wa leo, ambao umeathiri sekta muhimu kama vile uchukuzi, masoko, hospitali na mashule.
Makumi ya maelfu ya wananchi wa Sudan hapo jana waliandamana wakiitikia wito uliotolewa na Jumuiya ya Wafanyakazi wa nchi hiyo na muungano wa wapinzani, kupinga kuhukumiwa waandamanaji wanaodaiwa kukiuka sheria ya hali ya hatari iliyotangazwa nchini humo hivi karibuni.
Ripoti zinasema kuwa, askari usalama wa Sudan walitumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi kuwatanya waandamanaji mjini Khartoum na katika miji mingine ya nchi hiyo.
Sudan ilianza kugubikwa na maandamano ya wananchi tangu Disemba 19 mwaka jana kulalamikia hali ngumu ya kiuchumi na kupanda bei za bidhaa muhimu hususan mkate na petroli, maandamano yaliyogeuka na kuwa ya kumtaka Rais al-Bashir ajiuzulu.
Makumi ya waandamanaji ambao wanataka Rais Omar al-Bashir ang'atuke madarakani wametiwa mbaroni, huku ripoti za asasi za kiraia zikieleza kuwa watu 57 wameuawa hadi sasa katika ghasia na machafuko huko Sudan.