Muda wa hali ya hatari Sudan wapunguzwa huku maandamano yakishadidi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i52108-muda_wa_hali_ya_hatari_sudan_wapunguzwa_huku_maandamano_yakishadidi
Muda wa kutekelezwa sheria ya hali ya hatari nchini Sudan umepunguzwa kutoka mwaka mmoja na sasa ni miezi sita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 11, 2019 23:28 UTC
  • Muda wa hali ya hatari Sudan wapunguzwa huku maandamano yakishadidi

Muda wa kutekelezwa sheria ya hali ya hatari nchini Sudan umepunguzwa kutoka mwaka mmoja na sasa ni miezi sita.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, Bunge la Sudan jana lilitangaza kupunguza muda wa hali ya hatari kutoka mwaka mmoja na kuwa miezi sita.

Taarifa fupi ya Bunge la Sudan iliyozifikia duru za habari ilisema: Sheria ya kutekelezwa hali ya hatari ya mwaka mmoja imepunguzwa na kuwa miezi sita.

Sudan ilianza kugubikwa na maandamano ya wananchi tangu Disemba 19 mwaka jana wanaolalamikia hali ngumu ya kiuchumi na kupanda bei za bidhaa muhimu khususan za mkate na nishati yya mafuta.

Maandamano ya wananchi wa Sudan dhidi ya serikali ya Rais Omar al-Bashir

Tangazo la Bunge la Sudan la kupunguza muda wa utekelezwaji wa sheria ya hatari ya hatari kutoka mwaka mmoja hadi miezi sita linatolewa katika hali ambayo, nchi hiyo imeendelea kukumbwa na maandamano dhidi ya serikali karibu kila siku.

Maafisa wa polisi nchini Sudan wameendelea kuzima maandamano ya wananchi kwa kutumia mabomu ya kutoa machozi, sanjari na kuwatia mbaroni viongozi waandamizi wa vyama vya upinzani.

Hivi karibuni shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International lilitangaza kwamba watu karibu 60 wameuawa hadi sasa katika maandamano hayo.

Maandamano ya hivi sasa ya nchini Sudan ni makubwa zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Maandamano hayo yaliyoanza kwa kulalamikia ughali wa maisha sasa yamebadilika na kuwa ni wimbi la kumtaka Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo ang'oke madarakani, lakini bado anashikilia msimamo wake wa kubakia madarakani.