Maandamano ya upinzani yaendelea Sudan sambamba na kuapishwa baraza jipya la mawaziri
Wakati mawaziri wa serikali mpya iliyoundwa nchini Sudan wakiwa wanakula kiapo cha utiifu, mamia ya watu wameandamana katika miji miwili mikubwa ya nchi hiyo ya Khartoum na Omdurman.
Duru za habari zimeripoti kuwa mamia ya watu waliandamana jana katika mji mkuu Khartoum na katika mji wa pili kwa ukubwa wa nchi hiyo Omdurman, huku wakitoa miito ya shime ya "Uhuru, Amani na Uadilifu".
Askari wa usalama walitumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao.
Maandamano hayo yamefanyika huku mawaziri wa serikali iliyoundwa na waziri mkuu mpya Mohamed Tahir Ayala wakiapishwa mbele ya Rais Omar al Bashir, Ikulu hapo jana.
Hiyo ni serikali ya tatu kuundwa nchini Sudan katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita. Serikali mbili zilizotangulia zilivunjwa kwa kisingizio cha kushindwa kutatua mgogoro wa hali mbaya ya uchumi inayoikabili nchi hiyo.
Tangu katikati ya mwezi Desemba mwaka jana hadi sasa, Sudan inashuhudia maandamano makubwa ya kulalamikia hali hali mbaya ya uchumi na ongezeko la bei za bidhaa.
Maandamano hayo ambayo hayajawahi kushuhudiwa mfano wake katika miongo mitatu iliyopita nchini Sudan yamesababisha watu wasiopungua 40 kuuawa hadi sasa.
Licha ya kufanyika mabadiliko ya kuundwa baraza jipya la mawaziri, wapinzani wangali wanang'ang'ania msimamo wao wa kutaka rais Omar Al-Bashir aondoke madarakani.../