Maandamano dhidi ya Rais Omar al-Bashir yaendelea kushuhudiwa nchini Sudan
Maelfu ya raia wa Sudan jana walifanya maandamano katika miji mbalimbali ya nchi hiyo wakisisitiza kutekelezwa takwa lao la kuondoka madarakani Rais Omar Hassan al-Bashir wa nchi hiyo.
Maandamano hayo makubwa yamefanyika katika mji mkuu Khartoum na miji mingine muhimu ya nchi hiyo. Maandamano ya wananchi wa Sudan yanaendelea licha ya serikali mpya kuundwa chini ya Waziri Mkuu Muhammad Tahir Ayala.
Baadhi ya duru zimeliponda baraza jipya la mawaziri la Sudan zikisema kuwa, hakuna mabadiliko ya msingi yaliyofanyika kwani asilimia kubwa ya mawaziri wa Baraza la Mawaziri lililotangulia wamo katika serikali hiyo mpya.
Tangu katikati ya mwezi Desemba mwaka jana hadi sasa, Sudan imekuwa ikishuhudia maandamano makubwa ya kulalamikia hali hali mbaya ya uchumi na ongezeko la bei za bidhaa.
al bashir
Maandamano ya hivi sasa ya nchini Sudan ni makubwa zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika kipindi cha miaka 30 iliyopita. Maandamano hayo yaliyoanza kwa kulalamikia ughali wa maisha sasa yamebadilika na kuwa ni wimbi la kumtaka Rais Omar al Bashir wa nchi hiyo ang'oke madarakani, lakini bado anashikilia msimamo wake wa kubakia madarakani.
Makumi ya waandamanaji ambao wanataka Rais Omar al-Bashir ang'atuke madarakani wametiwa mbaroni, huku ripoti za asasi za kiraia zikieleza kuwa watu zaidi ya watu 50 wameuawa hadi sasa katika ghasia na machafuko huko Sudan.