Watu 15 wauawa katika shambulizi la kigaidi Mogadishu, Somalia
(last modified Thu, 28 Mar 2019 15:08:42 GMT )
Mar 28, 2019 15:08 UTC
  • Watu 15 wauawa katika shambulizi la kigaidi Mogadishu, Somalia

Kwa akali watu 15 wameuawa katika mripuko wa bomu lililokuwa limetegwa garini, nje ya hoteli na mikahawa katika eneo lenye shughuli nyingi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Meja Mohamed Hussein ambaye ni afisa wa polisi mjini Mogadishu ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, mripuko huo umetokea leo nyakati za adhuhuri na kwamba watu wengine 16 wamejeruhiwa.

Naye Abdikadir Abdirahman, Mkurugenzi wa Huduma za Ambulensi katika eneo hilo amesema yumkini idadi ya waliopoteza maisha katika mripuko huo ikaongezeka, kutokana na majeraha mabaya waliyoyapata wapita njia na watu waliokuwa kwenye mikahawa hiyo. 

Kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab kupitia msemaji wake wa operesheni za kijeshi, Abdiasis Abu Musab limetangaza kuhusika na hujuma hiyo ya leo, ambayo imetokea karibu na eneo palipotokea shambulizi jingine siku chache zilizopita, katika barabara ya Makkatul Mukarramah, ambapo makumi ya watu waliuawa.

Wananchi wakikimbilia usalama wao baada ya kutokeo mripuko wa bomu Mogadishu

Aidha haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya watu 15 kuuawa katika shambulizi jingine la kigaidi katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu. Saqar Ibrahim Abdallah, Naibu Waziri wa Leba na Masuala ya Jamii wa Somalia ni miongoni mwa watu waliouawa katika shambulizi hilo la Jumamosi iliyopita.

Tangu mwaka 2007 kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab limekuwa likifanya juhudi zenye lengo la kuipindua serikali kuu ya nchi hiyo ambayo inapata himaya kutoka kwa askari wa Umoja wa Afrika AMISOM.

 

Tags