UNICEF: Maisha ya watoto 500,000 wa Kilibya yapo hatarini
Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetangaza kuwa, maisha ya watoto 500,000 nchini Libya yapo hatarini kutokana na kuibuka mapigano mapya katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli.
Taarifa ya Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF imezitaka pande zinazopigana nchini Libya kujiepusha na hatua ya kuwatumia watoto kama askari vitani na wawalinde watoto wote kwa mujibu wa sheria za kimataifa za haki za binadamu.
Wakati huo huo, Shirika la Afya Duniani WHO limetangaza kuwa, watu 47 wameuawa katika siku tatu zilizopita za mapigano katika mji mkuu Tripoli baina ya mahjeshi ya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa na vikosi vitiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar.

Jeshi la Taifa la Libya linaloongozwa na Jenerali mstaafu Khalifa Haftar, Alkhamisi iliyopita lilianzisha operesheni kubwa za mashambulio dhidi ya mji mkuu Tripoli na mahali yalipo makao makuu ya Serikali ya Maafikiano ya Kitaifa inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj.
Mapigano katika mji mkuu huo wa Libya yangali yanaendelea licha ya kutolewa miito kimataifa ya kutaka yasimamishwe. Jenerali Haftar anadhibiti eneo la mashariki ya Libya pamoja na sehemu kadhaa za kusini mwa nchi hiyo.
Jumuiya mbalimbali za kieneo na kimataifa ukiwemo Umoja wa Mataifa zimeendelea kutoa miito inayozitaka pande hasimu nchini Libya kusitisha vita na mapigano.